Corona yafagia asilimia 35 ya biashara ndogo

Corona yafagia asilimia 35 ya biashara ndogo

Na PETER MBURU

MAKALI ya janga la Covid-19 yalilemaza pakubwa uchumi wa biashara ndogondogo nchini, ambapo asilimia 35 ya biashara zote zilifagiliwa kufikia Julai 2021.

Hii ni kulingana na ripoti ya hivi punde zaidi kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK), ambayo kwa mara ya kwanza imeonyesha jinsi biashara hizo za juakali, zinazojumuisha asilimia 98 ya biashara zote nchini, ziliathirika kati ya Februari 2020 na Julai 2021.

Ripoti hiyo ambayo ilitolewa Alhamisi imedokeza kuwa nyingi za biashara hizo – ambazo kwa kawaida huajiri hadi wafanyakazi tisa – zilifungwa, kukosa uwezo wa kuweka hazina, kupungukiwa na wateja na familia za wamiliki wake kuteseka kwa njaa.

Biashara husika ni kama maduka, biashara za vibanda, vinyozi, hoteli ndogo na nyingine ambazo wamiliki wake huzitumia kama chanzo cha mapato yao.

“Kufikia Julai 2021, ni asilimia 38 ya biashara za MSE tu zilizokuwa zimerejelea hali yao ya kabla ya janga la Covid-19 kimapato, lakini asilimia 62 bado zinapata mapato ya chini ikilinganishwa na Februari 2020. Vilevile, biashara zilizofungwa ziliongezeka 2021, huku asilimia 35 ya wamiliki wa biashara waliokua kazini kabla ya Covid-19 wakitokomea kufikia Julai 2021,” ripoti hiyo ikasema.

Hii ndiyo ripoti ya kwanza kuonyesha kiwango ambacho janga la Covid-19 limeathiri uchumi wa biashara za juakali nchini, na inaongeza kusema kuwa wengi wa wafanyabiashara hizo bado hawana imani kuwa mwaka huu hali itakuwa nzuri, kutokana na kupungua kwa idadi ya wateja.

Jumla ya asilimia 34 ya wamiliki wa biashara hizo kufikia Julai walisema kuwa hali ya biashara zao imezorota, ikilinganishwa na asilimia 11 waliotoa maoni sawia Novemba 2020.

Ripoti hiyo aidha inasema kuwa biashara nyingi nchini (asilimia 68) zimekuwa katika hali mbaya na kushindwa kuweka hazina ambayo inaweza kuziokoa wakati wa janga, kutoka asilimia 40 ambazo hazikuwa na hazina Februari 2020.

“Kufikia Julai, biashara nyingi ziliripoti kupokea nusu ya wateja ambao zilikuwa zikipokea Februari 2020,” ripoti hiyo ikasema.

Maisha yalipokuwa magumu kwa wamiliki wa biashara hizi, wengi wao walishindwa kutimiza majukumu ya kibinafsi kwa familia zao kama kuzipa chakula, ripoti hii ikionyesha kuwa takriban nusu ya familia za wamiliki wa biashara za juakali (asilimia 47) zilikuwa zikikosa chakula kufikia Julai 2021.

Hii ni ikilinganishwa na asilimia 14 ya familia zilizokuwa zikikosa Februari 2020, na asilimia 61 ambayo ndiyo kubwa zaidi kwa familia zilizokosa chakula- kati ya Aprili na Julai 2020.

Matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya Februari 2020 na Julai 2021 yamefichua mateso ambayo familia nyingi zilizokuwa zikitegemea biashara za Jua Kali nchini zimepitia kwa kipindi cha miezi 17, na ambayo bado hayajaisha kutokana na hali ya mfumko wa bei za bidhaa muhimu ambao umekuwepo mwaka huu 2021.

Shirika la Kukusanya Takwimu Kenya (KNBS) mnamo 2016 lilibaini kuwa biashara za juakali zinajumuisha asilimia 98 ya biashara zote Kenya.

Habari kuhusu nyingi za biashara hizi hazipatikani kwa kuwa hazijarasmisha shughuli zao, kwa kukosa usajili (asilimia 92) wala leseni (asilimia 65) na hivyo imekuwa vigumu kwa serikali kubaini hali yake.

CBK katika ripoti ya sasa ilibaini kuwa nyingi za biashara hizo sasa zimelazimika kubuni mbinu za kutumia mitandao kwa malipo na mauzo ya bidhaa, kama mbinu ya kupata hela zaidi na kuendelea kujikimu.

“Asilimia 70 ya wamiliki wa biashara ndogo zaidi mnamo Juali 2021 walisema kuwa walikuwa wakikubali malipo kidijitali, kutoka asilimia 59 waliokuwa wakikubali Februari 2020,” ripoti hiyo ikasema.

You can share this post!

Ajipata kizimbani kwa madai ya kuiba nakala mbili za Biblia

Michael Carrick aondoka Man-United baada ya kusimamia klabu...

T L