HabariSiasa

Corona yaingia Ikulu

June 15th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAFANYAKAZI wanne wa Ikulu ya Nairobi wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona Jumatatu alasiri.

Kwenye taarifa iliyotumwa na msemaji wa Ikulu Kanze Dena, watu hao walipatikana na virusi hivyo baada ya shughuli ya kila mara ya kuwapima wafanyakazi wa Ikulu, iliyofanyika Alhamisi Juni 11.

Maafisa hao sasa wamelazwa katika Hospitali ya Mafunzo na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) ambako wanatibiwa.

“Wafanyakazi wote wa Ikulu hupimwa, akiwemo Mheshimwa Rais na watu wa familia, kila mara kuhakikisha kuwa wao ni salama,” akaeleza Bi Dena.

Aliongeza kuwa watu wa familia za maafisa hao (walioambukizwa) pamoja na wale ambao walitangamana nao pia wamefuatiliwa na wanatibiwa.

Habari hizi zinajiri saa chache baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kujitokeza na kutangaza kuwa amethibitishwa kuwa hana virusi vya corona baada ya kupimwa Jumapili katika kituo cha Taasisi ya Uchunguzi wa Kimatibabu Nchini (KEMRI), Mbagathi.

“Ikulu ingependa kuwaarifu Wakenya kwamba Mheshimiwa Rais na familia yake wako salama na hawajaambukizwa na maradhi hayo. Vile vile, Ikulu ingependa kuwakumbusha Wakenya kuwa kila mtu ako katika hatari ya kuambukizwa Covid-19. Hakuna aliye na kinga dhidi ya maradhi hayo. Hivyo basi sisi sote tujizatiti kudumisha kikamilifu taratibu za Covid-19 ilivyoratibiwa na Wizara ya Afya.”