Habari Mseto

Corona yakosesha kazi Wakenya zaidi ya 300,000

May 22nd, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

ZAIDI ya Wakenya 300,000 wamepoteza ajira zao tangu kuzuka kwa virusi vya corona mnamo Machi, zimeonyesha takwimu kutoka kwa idara mbalimbali nchini.

Takwimu hizo ni kutoka kwa Shirika la Kitaifa la Kukusanya Takwimu (KNBS) na utafiti uliofanywa majuzi na Wizara ya Fedha.

Kuna hofu kwamba huenda watu wengine zaidi ya milioni moja wakapoteza ajira zao katika miezi kadhaa ijayo, hasa katika sekta ya juakali, ambayo huhusisha biashara ndogondogo na utengenezaji bidhaa.

Baadhi ya kampuni zinaendelea kuwafuta kazi wafanyakazi wake, zikitaja hali ngumu ya kiuchumi kutokana na janga hilo.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Ijumaa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa Waajiri Kenya (FKE), Bi Jacqueline Mugo, alisema kuwa kampuni nyingi bado zinaendelea kuiandikia barua Wizara ya Leba kuhusu mpango wa kuwafuta kazi wafanyakazi wake.

Miongoni mwa kampuni hizo ni mashirika zaidi ya 20 ambayo ni wanachama wa muungano huo.

“Mashirika kadhaa yameiandikia barua Wizara ya Leba kuhusu mpango wa kutaka kuwafuta kazi wafanyakazi wake. Tayari, baadhi ya mashirika yashawafuta kazi wafanyakazi wake, huku mengine yakiwatuma kwa likizo ya lazima yakingoja kuona ikiwa hali itaimarika,” akasema.

Kwenye hotuba yake mnamo Leba Dei, Rais Uhuru Kenyatta alionya kwamba huenda zaidi ya Wakenya milioni moja wakapoteza ajira zao kwa kipindi cha miezi sita ijayo kutokana na athari za janga hilo.

“Lazima tujitayarishe kwa mfumo mpya wa kimaisha, kwani hatujui muda ambao virusi hivi vitaendelea kuwa nasi. Miongoni mwa athari zake ni watu wengi kupoteza ajira zao, kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea mtangamano wa watu, hali ambayo ni miongoni mwa mambo yaliyoathiriwa ,” akasema Rais Kenyatta.

Hata hivyo, alitoa hakikisho kwamba serikali inafanya iwezavyo kuwalinda Wakenya dhidi ya athari za kiuchumi.

Wiki iliyopita, Waziri wa Leba, Bw Simon Chelugui, alitangaza mpango wa serikali kuanza kuwapa wafanyakazi waliopoteza ajira marupurupu maalum ya Sh5,000 kila mwezi kwa miezi mitatu ijayo, ili kuwasaidia kukabiliana na hali ngumu kimaisha.

Hata hivyo, Bw Chelugui alisema kuwa mpango huo utaanza kutelelezwa tu , baada ya serikali kuthibitisha idadi kamili ya wafanyakazi waliopoteza ajira zao.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na KNBS, baadhi ya sekta zilizoathiriwa sana ni utalii, hoteli na uchukuzi.

Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani alitaja hali hiyo kuchangiwa na marufuku ya safari za ndege za kimataifa ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.