Habari Mseto

Corona yaongezea msumari moto kwa kidonda cha wakuzaji wa makadamia

November 13th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wa makadamia kutoka kaunti ya Kiambu wanahesabu hasara baada ya kukosa soko la kuyauza kutokana na virusi vya corona.

Waliendelea kuteta mawakala wameharibu soko pakubwa kwani wanaenda katika mashamba yao na kununua zao hilo kwa bei ya kutupa.

Wakulima hao waliokongamana mjini Thika mnamo Alhamisi walitoka sehemu za Thika mjini, Gatundu ya Kaskazini na kusini, na Githunguri.

Wakati wa mkutano huo wakulima wengi walilazimika kutoa malalamiko yao na kueleza masaibu wanazopitia kwenye mashamba yao.

Bi Joyce Njeri kutoka eneo la kiganjo, alisema yeye kama mkulima amabaki na mazao mengi katika ghala lake huku wakingoja soko lirudi sawa.

“Hata ingawa mawakala wengi wamefika kwangu walitaka niwauzie kwa bei ya hasara nilikataa ombi lao. Nimekubali kuvumilia hadi wakati soko litarejea kuwa sasa,” alisema Bi Njeri.

Aliwashauri wakulima wenzake wawe watulivu na waache kukimbilia kuuza katika bei ya nchini.

Bw Lawrence Ndarwa ambaye pia ni mkulima kutoka Gatundu Kaskazini alisema hata yeye hataweza kuuza zao hilo kwa mawakala ambao wanataka kunyanyasa wakulima.

” Mimi kama mkulima wa macadamia kwa muda mrefu naelewa umuhimu wa zao hilo na kwa hivyo singependa kuleta mzaha wakati wa kuyauza katika soko,” alisema Bw Ndarwa.

Mkurugenzi wa kiwanda cha Jungle Nut Macadamia Ltd, mjini Thika Bw Patrick Wainaina, alisema homa ya covid- 19 imeathiri uuzaji wa zao hilo pakubwa ambapo hata masoko ulimwenguni yanauza kwa bei ya nchini.

” Hata bei ya macadamia imetoka kwa Sh 200 kwa kilo hadi Sh 60 jambo ambalo ni hasara kubwa kwa wakulima,” alisema Bw Wainaina.

Alisema itachukua muda fulani kabla ya mambo kurejea kama kawaida, lakini hata hivyo wakulima ni sharti wavumilie kwa sasa.

Alitoa mwito kwa vijana hasa katika mashinani wajitokeze wazi na kuanza kupanda macadamua kwa wingi kwa sababu imepiku zao la chai na kahawa katika mapato ya kifedha.