Corona yaponda miji na vijiji

Corona yaponda miji na vijiji

Na WAANDISHI WETU

WINGU la maangamizi limetanda kote nchini huku aina mpya ya corona maarufu kama ‘Delta’ ikiua watu kwa mamia.

Uchunguzi wa Taifa Leo umeonyesha kuongezeka kwa vifo katika muda wa wiki chache zilizopita katika maeneo mengi ya nchi kutokana na maradhi hayo.

Tofauti na ilivyokuwa awali ambapo virusi hivyo vilisambaa sana katika miji mikuu, sasa wakazi wa vijijini pia wameanza kushuhudia magonjwa na vifo vingi katika hali ya kutisha.

Familia katika maeneo tofauti ya nchi zimekuwa zikiripoti jinsi zinavyokumbwa na changamoto wakati kijiji kizima kinapoandamwa na vifo karibu kila wiki, hali inayozua maswali kuhusu ukweli wa takwimu zinazotolewa na Wizara ya Afya za maambukizi na vifo.

Wengi wa watu waliozungumza na Taifa Leo walieleza kupoteza watu wengi wa familia, marafiki na majirani katika siku za hivi majuzi.

“Kwa sasa nina watu sita ambao baadhi ni wa familia, majirani ama marafiki ambao miili yao iko mochari ikisubiri kuzikwa,” alieleza Eliud Gatobu, mkazi wa Nairobi.

Mnamo Jumatano, serikali ya Amerika ilitoa tahadhari kwa raia wake kutokana na maambukizi kuongezeka.

Mnamo Alhamisi, hoteli ya Breeze View iliyoko mjini Mpeketoni, Kaunti ya Lamu ilifungwa baada ya wengi wa wafanyakazi wake kuambukizwa virusi vya corona.

Mmiliki wa hoteli hiyo, John Wanyoike Kiuna, alithibitisha hayo baada ya kutolewa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), ambapo alikuwa amelazwa kwa zaidi ya wiki mbili.

“Janga la Covid-19 sasa limekuwa doa jeusi katika utoaji wa huduma hotelini kwangu. Kwa sasa imefungwa. Mimi mwenyewe bado niko kwenye safari ya kupona,” akasema Bw Wanyoike.

Aliiomba serikali kuingilia kati na kusaidia wafanyabiashara na familia zilizoathiriwa na janga la corona moja kwa moja, akisema gharama ya matibabu ya Covid-19 ni ya juu mno.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Lamu, Dkt Anne Gathoni alisema, idadi ya maambukizi inaendelea kuongezeka Lamu na hilo limechochea wananchi kujitokeza kwa wingi wakitaka wapewe chanjo.

Siku chache zilizopita, serikali za kaunti za Kilifi na Mombasa zililazimika kutoa tahadhari kwa wakazi kuhusu ongezeko la maambukizi, huku wahudumu wa afya wakisema vyumba vya kulaza wagonjwa wa Covid-19 vimejaa pomoni.

Katika eneo la Mlima Kenya, wananchi wamelaumiwa kwa kupuuza kanuni za kuepusha maambukizi.

Eneo hilo ambalo hivi majuzi lilishuhudia shughuli nyingi za kampeni za chaguzi ndogo, ni miongoni mwa maeneo ambayo yanakumbwa na maambukizi na vifo vingi vijijini.

Katika Kaunti ya Nakuru, vifo visivyopungua 50 viliripotiwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita pekee. Wagonjwa 101 walithibitishwa kuwekewa mashine za kuwasaidia kupumua, huku saba wakiwa wamelazwa ICU.

Maeneo ya mashambani ya Njoro, Gilgil, Rongai, Subukia, Naivasha, Olenguruone na Solai, kando na mitaa ya mabanda yameathirika zaidi.

“Idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini na vifo Nakuru imeongezeka sana katika wiki mbili zilizopita. Ninaomba wakazi wasilegeze kamba kwa sababu aina ya virusi ya Delta inasambaa kwa kasi mno,” akasema Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui.

Wiki iliyopita, watu watano kutoka kijiji kimoja kilicho eneo la Njoro walifariki baada ya kuonyesha dalili za kuugua Covid-19.

Hali sawa na hii inashuhudiwa katika Kaunti ya Nyeri ambapo watu 38 walifariki kwa Covid-19 Julai.Hivi majuzi, walimu sita katika Shule ya Upili ya Nyeri waliambukizwa virusi vya corona.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya katika Kaunti ya Nyeri, Bw Nelson Muriu alisema shule zimetambuliwa kuwa sehemu hatari za maambukizi kwa sababu watu ni wengi, na inahofiwa wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Kwanza pia huenda baadhi yao walikuwa wameambukizwa bila kujua.

Katika Kaunti ya Meru, wafanyakazi wote waliagizwa kufanyia kazi nyumbani isipokuwa wale wanaotoa huduma za dharura kama vile katika idara za afya na usalama ili kuepusha msambao wa virusi.

Idara ya afya ya umma katika kaunti hiyo ililazimika kuagiza wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Maritati iliyo Buuri, wasiende shuleni kwa siku 14 baada ya walimu saba kupatikana wameambukizwa.

Kituo cha Polisi cha Gathoge, kilicho katika Kaunti ya Kirinyaga, kilifungwa baada ya maafisa wote wanaohudumu hapo kupatikana wanaugua Covid-19.

Ripoti za Kalume Kazungu, Winnie Atieno, Nicholas Komu, Irene Mugo, George Munene, Eric Matara na David Muchui

You can share this post!

Hatimaye msimu mpya wa EPL waanza leo

Jamii yaiomba korti izuie operesheni za serikali Laikipia