Habari Mseto

Corona yasababisha matatizo ya akili

June 20th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

IDADI ya watu wanaopata matatizo ya kisaikolojia kutokana na janga la corona imeongezeka na hii ni tisho kwa vita dhidi ya virusi hivyo, wizara ya Afya imesema.

“Janga la corona ni tisho kwa umma. Linasababishia watu matatizo ya kisaikolojia. Tunaelezwa baadhi ya kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi hivi kunanyima watu maisha yao ya kijamii na hii inawaathiri kisaikolojia na ndio sababu serikali imezingatia utoaji ushauri nasaha kwao,” waziri msaidizi wa afya Rashid Aman alisema.

Hata hivyo, alieleza kuwa serikali inajitahidi kuwasaidia wanaokabiliwa na matatizo hayo.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth alisema watu wengi wanaotafuta msaada kwa kupata matatizo ya kisaikolojia ni vijana. Serikali imewahimiza watu kupiga simu kwa 1199 kupata ushauri wa matatizo ya kisaikolojia.

“Watu wamekuwa wakitumia nambari hii na wengi ni vijana wanaolalamikia wasiwasi na hofu. Tunahimiza watu kuitumia,” alisema Dkt Amoth. Dkt Amoth alisema kwamba watu wanaopata matatizo ya akili huwa wanadhulumiwa na kupuuzwa katika jamii. “ Hii huwa inawaweka katika hatari ya kuambukizwa corona,” alisema.

Idadi ya watu walioambukizwa corona imefikia 4,478 baada ya visa vipya 104 kuthibitishwa jana huku maafisa watatu wa polisi kutoka kituo cha Kamukunji na wahudumu wa afya 30 kutoka hospitali ya Pumwani jijini Nairobi wakisemekana kuwekwa karantini kwa kupatikana na virusi na kutangamana na waathiriwa.

Kwenye taarifa ya kila siku kuhusu hali ya corona nchini, wizara ya afya haikutaja moja kwa moja visa hivyo lakini ikasema kila mtu anayetangamana na waathiriwa wa corona huwa anawekwa karantini. Dkt Amoth alisema kwamba ili kuzuia maambukizi katika magereza nchini, serikali imeweka vituo vya kutenga wafungwa wanaothibitishwa kuwa na corona.

“ Tumeshirikiana na idara ya magereza na tumeanzisha vituo vya kutenga wafungwa wanaothibitishwa kuwa na corona katika magereza yote nchini,” alisema.

Mnamo Ijumaa, mahakama ya Mombasa ilifungwa kwa muda usiojulikana baada ya wafanyakazi 11 kuambukizwa corona na wengine 115 waliotangamana nao kuwekwa karantini.