Siasa

Corona yasimamisha 'Reggae' Pwani

November 10th, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

KIVUMBI cha kisiasa kilichoanza kushika kasi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Msambweni kimeanza kufifia kufuatia agizo la serikali kusitisha mikutano ya kisiasa.

Rais Uhuru Kenyatta alitoa agizo hilo wiki jana na kuelekeza wanasiasa nchini kusitisha mikutano ya hadhara kwa siku 60 ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Tayari, mgombeaji wa kiti cha ODM, Omar Boga ametangaza kuwa ameambukizwa corona na yuko karantini.Rais Kenyatta alisema kuwa, wanasiasa wataruhusiwa kufanya mikutano katika kumbi ambazo zitaruhusu watu wachache pekee.

Agizo hilo, hivyo basi limefifisha ubabe wa kisiasa uliokuwa unatazamiwa kujitokeza kati ya Naibu Rais William Ruto na mpinzani wake kinara wa ODM Raila Odinga.

Wawili hao walitarajiwa kuongoza kampeni katika eneo bunge hilo ili kuwapigia debe wawaniaji wanaowaunga mkono kwenye uchaguzi huo ambao utafanyika mnamo Disemba 15.

Bw Odinga anampigia debe Omar Boga ambaye ndiye anapeperusha bendera ya chama cha ODM huku Bw Ruto naye akiegemea upande wa Feisal Bader ambaye anawania kiti hicho kama mgombeaji huru.Tayari, washirika wa wawili hao walikuwa wameanza kampeni za kuwapigia debe wawaniaji wao.

Upande wa Bw Ruto unaongozwa na waliokuwa maseneta Johnson Muthama (Machakos), Hassan Omar (Mombasa) na Boni Khalwale wa Kakamega.Kundi hilo limekuwa likiendeleza siasa eneo hilo kwa muda wa wiki mbili mfululizo sasa.

Wanasiasa wa ODM wakiongozwa na katibu wa chama Edwin Sifuna pia walikuwa wamepigga kambi eneo hilo.Kufuatia agizo hilo, pande zote mbili zimetangaza kusitisha siasa zake za mikutano ya hadhara.

Bw Ruto amesema atafanya hilo hadi pale ataeleza wafuasi wake tofauti. “Nimeamua kusitisha mikutano mpaka baadaye. Mikutano ambayo ilikuwa nimepanga katika kaunti tofauti pia nimesitisha,” akasema Bw Ruto kwenye mtandao wake wa Twitter.ODM nao walisema kuwa watafuata agizo la serikali kama lilivyotangazwa na Rais Kenyatta.

“Leo tumechangisha pesa kwa ajili ya kampeni zetu za maeneo bunge ya Msambweni, Wundanyi/Mbale, Kisumu Kaskazini na Dabaso kwa ajili ya uchaguzi wa Disemba 15. Katibu wetu Edwin Sifuna ametangaza kuwa kampeni zetu zitafanywa chini ya kanuni mpya ambazo zimetangazwa,” ilisema taarifa ya ODM.

Kampeni hizo zimeanza kuchukua mkondo mpya huku wale wanaongoza kampeni wakionekana kufuata agizo la serikali la kufanya mikutano kwenye kumbi.

Hali hiyo tayari imeondoa mihemko ya kisiasa ambayo huletwa na mikutano ya siasa inayozua hisia tofauti.Kwa sasa, itasubiriwa kuonekana ni vipi siasa hizo zitaendelea hadi siku ya kura huku ikiwa wazi kuwa wale wanaowania watapata wakati mgumu kuuza sera zao.

Wengine wanaowania kiti hicho ni pamoja na wale wa vyama huru, Bi Sharlet Mariam Akinyi, Mansury Kumaka, Charles Bilali, Shee Abdulrahman (Wiper), Ali Hassan Mwakulonda (Party of Economic Democracy), Marere Wamwachai (National Vision Party) and Khamis Mwakaonje (United Green Movement).

Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na mwenzake wa Kwale, Salim Mvurya pia walikuwa wameahidi kuonyeshana kivumbi. Bw Joho anamuunga Bw Boga naye Mvurya anampigia debe Bw Bader.

Tayari, uhasama wa kisiasa ulikuwa umeanza kujitokeza kati ya magavana hao wawili kuhusiana na uchaguzi huo mdogo. ? Bw Mvurya alikuwa amemuonya Bw Joho na kusema kuwa hatakubali kaunti yake ya Kwale itumike kama ‘kiwanja cha vita’ akimaanisha siasa za ubabe ambazo Bw Joho ametambulika nazo.

Kwa sasa, itasalia kutazamwa namna viongozi hao watakavyomenyana kisiasa kwenye uchaguzi huo mdogo ambao wengi wamesema kampeni zake zimekosa makali kufuatia kusitishwa kwa mikutano ya hadhara.