Corona yasukuma watoto kushiriki katika ugaidi – UN

Corona yasukuma watoto kushiriki katika ugaidi – UN

Na MASHIRIKA

NEW YORK, AMERIKA

JANGA la corona linasukuma watoto kutoka familia masikini katika maeneo yanayokumbwa na mizozo, hasa barani Afrika, kujiunga na makundi yenye silaha yakiwemo ya kigaidi, afisa wa cheo cha juu wa Umoja wa Mataifa alionya Ijumaa.

Idadi ya watoto wanaosajiliwa na makundi ya wapiganaji haijulikani lakini kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, mnamo 2019 pekee, watoto wapatao 7,740 baadhi wakiwa na umri wa miaka sita, walisajiliwa na makundi ya waasi kutumiwa kama wapiganaji au kutekeleza majukumu mengine.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa dhidi ya watoto kutumiwa kama wapiganaji, maarufu kama Red Hand Day, Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na Mizozo yenye silaha, Virginia Gamba, alisema idadi ya watoto wanaosajiliwa na makundi haramu huenda ikaongezeka kutokana na hali ngumu inayosababishwa na corona.

“Kuna tisho halisi kwamba jamii zinapokosa ajira na nyingi kuendelea kutengwa kwa sababu ya athari za corona kwa uchumi na jamii, tutashuhudia idadi ya watoto wanaosajiliwa na makundi haramu ikiongezeka,” alisema.

Akaongeza: “Watoto wengi watavutiwa au mara nyingine kuambiwa na wazazi wao waende tu na kujiunga na makundi hayo kwa sababu lazima wawe na mtu wa kuwalisha.”

Wavulana na wasichana wenye umri mdogo bado wanalazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha kama wapiganaji, wapishi au watumwa wa ngono.

Umoja wa Mataifa umeorodhesha nchi 14 zikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Sudan Kusini na Somalia miongoni mwa nchi ambazo watoto wanasajiliwa kujiunga na makundi yenye silaha.

Mwaka jana, shirika hilo lilihimiza mapigano yasitishwe kote ulimwenguni kusaidia kukabili corona lakini makundi yenye silaha yanaendelea kupigana.

Gamba aliambia Thomson Reuters Foundation kwamba, janga hili limetatiza juhudi za kulinda watoto katika maeneo yanayokumbwa na vita.

Afisa huyo alisema, ana wasiwasi kuhusu mashambulizi ya magaidi dhidi ya watoto katika nchi za eneo la Ziwa Chad na jangwa la sahara. Magaidi wa Kiislamu wamekuwa wakiwateka, kuwaua watu wakiwemo watoto na kuwafanya wengi kutoroka makwao.

“Kwa kuwa watoto hawako shuleni, wanalengwa waliko ili watekwe au kusajiliwa kujiunga na makundi hayo,” alisema Gamba. Kabla ya janga la corona, makundi hayo yalikuwa yakishambulia shule na kuteka wanafunzi wanaowafanya wapiganaji au kuwashirikisha katika shughuli nyingine haramu.

You can share this post!

2022: Joho awakashifu wanaokejeli azma yake

UMBEA: Utandawazi usitutoe fahamu tusahau msingi wa...