Michezo

CORONA YATEKA EPL: COVID-19 yasababisha mechi kusitishwa

March 14th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

NI rasmi sasa kwamba Ligi Kuu ya soka nchini Uingereza (EPL) haitaendelea jinsi ilivyoratibiwa wikendi hii, kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona nchini humo na kote duniani.

Klabu za Arsenal, Bournemouth, Chelsea, Everton, Leicester, Manchester City, Watford na West Ham United zimeshuhudia angalau mchezaji ama afisa akitengwa ili kudhibiti uenezaji wa ugonjwa huo wa COVID-19.

Mechi zote za Ligi Kuu sasa zimeahirishwa hadi Aprili 4.

Mkutano wa dharura uliandaliwa Ijumaa ambapo klabu zote za EPL ziliamua kwamba mechi zisukumwe mbele kwa majuma matatu, baada ya vikosi vya Arsenal, Chelsea na Everton kuwekwa katika karantini ili kuzuia maambukizi.

Mechi kati ya Arsenal na Brighton & Hove Albion hii leo ilikuwa miongoni mwa 20 zilizokuwa zimepangwa kuchezwa wikendi hii na ijayo, lakini sasa zimefutiliwa mbali.

Kocha Mikel Arteta ni mmoja wa maafisa aliyepatikana na virusi vya corona. Sasa atajitenga mbali na watu ili kuzuia maambukizi.

Vilevile, inatarajiwa kuwa kikosi kizima cha Arsenal pamoja na benchi ya kiufundi pia zitachukua hatua sawa na hiyo.

Aidha, wanabunduki hao walifunga uwanja wao wa mazoezi wa London Colney baada ya Arteta kugunduliwa kuwa ameambukizwa corona.

Arteta alisema: “Inanisikitisha sana, lakini niliamua kupimwa nilipojihisi vibaya. Nitarejelea majukumu yangu mara tu nitakapopata nafuu na idhini.”

Mkurugenzi mkuu wa Arsenal, Vinai Venkatesham aliongeza: “Afya ya watu wetu na umma kwa jumla ni muhimu sana na tunachukulia hali hii kwa uzito unaofaa.”

Mechi kati Manchester City na Arsenal iliyoratibiwa kusakatwa uwanjani Etihad, katikati ya wiki Jumatano ndiyo ilikuwa ya kwanza kuahirishwa Uingereza.

Wachezaji wa Arsenal walikuwa wamekutana na mmiliki wa klabu ya Olympiakos, Evangelos Marinakis ambaye alipimwa baadaye na kubainika kuwa na virusi hivyo vinavyosababisha homa hatari.

Huku michezo mingine na mataifa mbalimbali yakitangaza kusimamisha ligi zao kama tahadhari, EPL awali ilikuwa imetoa taarifa kabla ya Arteta kupatikana na ugonjwa huo, ikisema kuwa mechi za wikendi hii zingeendelea jinsi ilivyopangwa.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson alikuwa amesisitiza kwamba kuahirisha mashindano ya michezo hakukuwa katika mipango yao.

Kampuni inayosimamia soka yote – ligi kuu, ligi ya daraja la pili, soka ya wanawake, soka ya mashinani – nchini Uingereza, EFL pia ilikuwa imetangaza Alhamisi jioni kuwa mechi za wikendi hii zingeendelea huku taarifa kama hiyo ikitolewa nchini Scotland.

Hata hivyo, baada ya hali ya Arteta kuthibitishwa, Ligi Kuu (EPL) ililazimika kupiga abautani baada ya kufanya mkutano wa dharura.

Tukienda mitamboni, kocha David Moyes wa West Ham pia alikuwa amejiweka katika karantini baada yake kusalimiana na Arteta timu zao zilipocheza uwanjani Emirates wikendi iliyopita.