Habari

Corona yatikisa nchi

March 15th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

TANGAZO la Serikali kwamba virusi vya corona vimetua nchini limetikisa nchi na kubadilisha hali ya maisha ya Wakenya huku wakichukua hatua tofauti kuepuka maambukizi zaidi.

Kufuatia tangazo hilo, asasi mbalimbali za umma na za binafsi, makanisa na vyuo, zimechukua hatua za kuhakikisha zimelinda Wakenya dhidi ya virusi hivyo.

Kwa mara ya kwanza, makanisa yalilazimika kulegeza misimamo na kaida za ibada katika hatua za kuzuia maambukizi.

Makanisa mengi, yakiwemo ya Seventh Day Adventist (SDA), Kanisa Katoliki na ya Kievanjelisti yaliwashauri waumini kubaki nyumbani iwapo wanahisi kuwa wagonjwa.

“Unashauriwa kukaa nyumbani ukijihisi mgonjwa,” Kanisa la SDA lilisema kwenye taarifa.

Viongozi wa makanisa mengi walipinga marufuku salamu za kutakiana heri, maji ya baraka na sakramenti kama njia ya kukinga waumini na mapadri.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Maaskofu wa Katoliki Nchini (KCCB) waliagiza makasisi kudumisha kiwango cha juu cha usafi wakati wa ibada.

Kinyume na hapo awali ambapo ilikuwa ni sharti kwa waumini kuhudhuria misa na ibada, makanisa yaliwaruhusu waumini walio na dalili za ugonjwa huo kama vile kukohoa na kupiga chafya, kukaa nyumbani hadi wapate nafuu.

“Tunamhimiza yeyote anayeugua mafua kutohudhuria ibada kimaksudi hadi watakapopata nafuu. Tunatambua shauku la Wakristo wengi kupokea Yukaristi kwa unyenyekevu hususan mdomoni. Kwa sasa, kutokana na tishio hili, tunawasihi waumini kuipokea mikononi. Hii itaendelea hadi virusi hivyo vitakapodhibitiwa,” ilisema KCCB.

Kanisa la Purpose Center Church pia lilijiunga kutoa mwelekeo kwa wafuasi wake.

Katika kanisa la Deliverance Umoja, ibada zilitarajiwa kuendelea kama kawaida huku wasimamizi wakiweka mikakati kabambe ya kuhakikisha usalama wa wafuasi wake.

Kanisa la SDA liliwashauri waumini wake wawe wakihudhuria ibada kwa hiari kuanzia Machi 14 pamoja na kutumia Mpesa kutuma sadaka na zaka zao.

Hayo yalijiri huku mikakati ya kukabiliana na tishio la kuzuka kwa mkurupuko wa virusi ikishika kasi nchini.

Maisha ya wakazi wa kaunti ya Mombasa yanatarajiwa kubadilika pakubwa baada ya serikali ya kaunti kupiga marufuku shughuli za burudani usiku.

Gavana Hassan Joho na Kamishna wa kaunti hiyo walisema marufuku hiyo itadumu kwa siku 30.

Katika kaunti ya Nyandarua, idara ya kukabiliana na dharura imetenga vitanda 22 na ambulensi mbili zitakazotumika kwa visa vya dharura.

Hospitali ya Meru Level Five sasa ina vitanda 20 na wadi ya kutenga wagonjwa kama sehemu ya kujiandaa kukabiliana na janga hilo.

Baraza la wazee la Njuri Ncheke lilisimamisha shughuli zake katika kaunti ya Tharaka Nithi na Meru kufuatia hofu ya ugonjwa huo.Hali ilikuwa sawa katika kaunti za Magharibi mwa Kenya na zilizo katika mipaka.

Uchunguzi wa ‘Taifa Jumapili’ ulibaini kwamba maduka ya jumla na ya kuuzia dawa hayakuwa na jeli za kunadhifisha mikono.

Kaunti za Kericho na Bomet pia zilishuhudia uhaba wa bidhaa hizo huku mamia ya wakazi wakipiga foleni katika vituo mbalimbali ili kuzinunua.

Jijini Nairobi, Chuo cha African Nazarene kilifungwa ili kuepuka kuenea kwa maradhi hayo.

Uongozi wa chuo kikuu cha Kisii, ulikashfu habari za uongo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa wanafunzi wawili wa chuo hicho walikuwa wameambukizwa Covid-19.

Naibu Chansela wa chuo hicho, Profesa John Akama, alipuuzilia mbali habari hizo na kusema kwamba, uvumi huo ulikuwa ukisambazwa na watu wenye nia mbaya kuhusu chuo hicho.

 

Na Mary Wangari, Benson Matheka, Winnie Atieno,Wycliffe Nyaberi, Victor Raballa, Sharon Achieng, Vitalis Kimutai, Dickens Wasonga, Ian Byron, George Odiwuor, Dianah Shimuli, Lenny Otieno, Nisa Nancy, Waikwa Maina, na David Muchui