Habari

Corona yatua mitaani

April 19th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

VIRUSI vya corona sasa vinapatikana katika mitaa yote jijini Nairobi na vinasambazwa hata na watu wasio na dalili ya kuwa navyo, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema Jumamosi.

Na kuanzia sasa, wahudumu wote wa afya wameagizwa kutohudumia mgonjwa bila kujikinga.

Kwenye hotuba yake jana katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Nairobi, Bw Kagwe alisema watu zaidi ya 100 walioambukizwa virusi hivyo Nairobi wanatoka kila kona ya jiji, ikiwemo mitaa kunakoishi matajiri na watu mashuhuri.

“Hakuna mtaa jijini Nairobi ambao haukosi mtu anayeweza kusambaza corona. Rekodi zetu zinaonyesha kuwa, mtu yeyote unayekutana naye anaweza kukuambukiza,” alisema.

Alisema katika mtaa wa Kilimani, kumeripotiwa kuwa na watu sita wanaougua corona, Kawangware (3), Karen (5), Pipeline ( 5), Utawala (4).

Visa vingine vimethibitishwa katika mitaa ta Mlolongo, Esteligh, Buruburu, Tasia, Parklands, Donholm, Hurlinghum, Makadara na Ngara.

“Kwa sababu ya hali hii, tunawashauri wahudumu wote wa afya na wote wanaofanya kazi vituoni wakiwemo wanaofagia, kuchukua hatua za tahadhari na kujikinga kila wakati. Usipokee mgonjwa bila vifaa vya kujikinga kwa sababu sasa vinapatikana kila mahali,” alisema Bw Kagwe.

Kufikia jana, idadi ya watu walioambukizwa nchini iliongezeka hadi 262 baada ya watu 16 zaidi kuthibishwa kuwa na virusi hivyo, tisa wakiwa wakazi wa Nairobi.

Bw Kagwe alisema watu hao walioambukizwa virusi hivyo humu nchini kwa sababu hawakuwa wamesafiri nje ya nchi. Idadi ya waliouawa na virusi hivyo ilifikia 12 baada ya mtu mmoja kufariki jana. Bw Kagwe alisema mmoja wa waliothibitishwa kuwa na virusi ni mganga mwenye umri wa miaka 84.

Waziri alihusisha ongezeko la maambukizi na tabia ya Wakenya kupuuza kanuni na maagizo ya serikali na hata wanaotengwa kutoa hongo watoroke vituoni kabla ya kumaliza muda unaohitajika.

Alisema kuwa watu hao ni hatari kwa jamii na akaonya kuwa wao na wanaowasaidia watachukuliwa hatua kali za kisheria. Bw Kagwe alitaja kaunti ya Mandera akisema Gavana wa kaunti hiyo, Ali Roba alimfahamisha kuwa watu kadhaa waliokuwa wametengwa walitoroka baada ya kutoa hongo.

“Nina habari kwamba, baadhi ya watu walio katika vituo vya kutenga wanaochunguzwa corona wamekuwa wakitoa hongo ili waondoke vituoni. Kwa mfano, leo hii gavana wa Mandera alinifahamisha kwamba, kuna watu waliotoa hongo wakaruhusiwa kuondoka. Waliowasaidia watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Bw Kagwe.

Wiki jana, iliripotiwa kuwa watu 32 waliokuwa wametengwa katika kaunti ya Mandera walikuwa wametoroka katika njia isiyoeleweka. Bw Kagwe alisema imefichuliwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia ujanga kukiuka amri ya kutoingia na kutoka nje ya kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale.

Alitoa mfano wa watu waliosafiri kutoka Nairobi hadi kaunti ya Homa Bay wakiwa na jeneza kwenye gari ili kujifanya walikuwa wakienda kwa mazishi.

“Katika kizuizi kimoja cha barabaranii, maafisa walishuku na kuwataka wafungue jeneza ikagunduliwa haikuwa na mwili na wakatengwa. Leo hii nimepokea ripoti kutoka Gavana wa kaunti ya Homa Bay kwamba, dereva wa gari hilo alipatikana na virusi vya corona. Inasikitisha mtu kutoka Nairobi alipeleka virusi vya corona kaunti ya Homa Bay na sasa tuko na kisa cha kwanza katika kaunti hiyo,” alisema Bw Kagwe.

Alisema madereva wa matatu pia wamekuwa wakitumia ujanja kusafirisha watu nje ya Nairobi na kaunti nyingine kinyume na agizo la serikali. Bw Kagwe alisema Wakenya watajuta wakiendelea kukosa nidhamu na kupuuza masharti yaliyowekwa na serikali kuzuia maambukizi ya corona.

Bw Kagwe aliwataka watu kupiga ripoti kwa maafisa wa serikali wakiona mtu aliyetoka jijini au maeneo yaliyofungwa kwa sababu ya corona.