Michezo

Corona yaua kocha

March 16th, 2020 2 min read

NA MASHIRIKA

MESTALLA, UHISPANIA

USIMAMIZI wa klabu ya Valencia umesisitiza kwamba vinara na wachezaji watano wa kikosi hicho cha soka ya Uhispania wako katika hali shwari ya kiafya licha ya kuugua homa kali ya corona.

Ezequiel Garay wa Valencia na timu ya taifa ya Argentina, alikuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kupatikana na virusi vya corona baada ya kufanyiwa vipimo vya afya mapema Jumapili. Baadaye siku hiyo, beki Eliaquim Mangala ambaye kwa sasa ametengwa, pia alipatikana na virusi hivyo.

Uhispania ndilo taifa la pili baada ya Italia ambalo limeathiriwa pakubwa na janga na corona barani Ulaya. Mnamo Alhamisi iliyopita, kivumbi cha La Liga kilisitishwa kwa muda usiojulikana baada ya wanasoka wa kikosi cha Real Madrid kutengwa ili kuzuia maambukizi zaidi ya gonjwa ambalo tayari limetangazwa kuwa janga la kitaifa nchini Uhispania.

“Ni wazi kwamba nimeanza mwaka huu wa 2020 kwa nuksi. Nimefanyiwa vipimo vya afya na kupatikana na virusi vya corona. Ingawa naendelea vyema, nazingatia ushauri wa madaktari na nimetengwa,” akaandika Garay, 33, kwenye mtandao wake wa Instagram.

Kwa upande wake, Mangala ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester City aliandika: “Nimejua leo kwamba nina virusi vya corona. Japo kwa sasa sijaona dalili zote za ugonjwa huo, nimejitenga nyumbani na siruhusiwi kutangamana na familia yangu,” akasema Mangala.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Valencia, baadhi ya wachezaji na wafanyakazi walioathiriwa wametengwa na wanaendelea kutibiwa chini ya uangalizi wa maafisa wa afya.

“Tuna imani kwamba tutalishinda janga hili iwapo tutadumisha umoja na kuwajibika ipasavyo. Kikosi kinajitahidi kadri ya uwezo kuhakikisha kwamba tunazuia maambukizi zaidi,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa upande wa Real, mchezaji wao mmoja wa timu ya vikapu aliyekuwa akiugua corona alitumia vifaa vya mazoezi vya timu ya soka na hivyo kuweka kikosi kizima katika ulazima wa kutengwa.

Wachezaji wengi wa soka nchini Italia wamepatikana na virusi vya corona, akiwemo mvamizi Patrick Cutrone anayechezea Fiorentina kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Wolves ya Uingereza.

Klabu ya Atalanta nchini Italia pia imeweka mikakati itakayoshuhudia wafanyakazi na wachezaji wake pia wakitengwa baada ya kuchuana na Valencia katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne iliyopita mjini Mestalla, Uhispania.