Habari

Corona yavamia bunge

June 30th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amekiri kuwa wabunge wawili wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19 na wala sio sita ilivyoripotiwa awali.

Kwenye taarifa aliyoitoa bungeni Jumanne alasiri, Bw Muturi amesema mbunge wa kwanza tayari ameondoka hospitalini na sasa amejitenga nyumbani kwake.

Bila kutaja majina yao, Spika amesema mbunge wa pili naye amelazwa hospitalini na anapokea matibabu katika wadi ya kawaida.

“Tofauti na habari ambazo zimekuwa zikisambazwa katika vyombo vya habari kuanzia juzi, habari ambazo Afisi ya Spika imepokea kufikia leo (Jumanne) Juni 30, 2020, ni kwamba wabunge wawili wamethibitishwa kuambukizwa na virusi vya corona,” Bw Muturi akasema.

Amesema habari kuhusu hali ya afya ya watu binafsi, wakiwemo wabunge, ni za siri na zinapasa kusalia kuwa kusalia kwa daktari, mgonjwa mwenyewe na familia yake.

“Kwa hivyo vyombo vya habari vinapasa kukoma kusambaza habari kuhusu visa vya maambukizi ya virusi vya corona bunge kana kwamba ni tofauti na visa vinginevyo vinavyotokea sehemu mbalimbali nchini,” Bw Muturi akasema.

Mnamo Jumatatu, gazeti moja la humu nchini liliripoti kwamba hofu imetanda bunge baada ya wabunge sita kuthibitishwa kuwa na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Kulingana na gazeti hilo, wabunge wangine waliotagusana na wabunge hao walishauriwa waende wapimwe, hali ambayo iliibua hofu kwamba idadi ya wabunge wenye virusi hivyo huenda ikapanda zaidi.

Jana, Muturi alisema Bunge linatekeleza masharti ya kuzuia maambukizi ya Covid-19 yaliyotangazwa na Wizara ya Afya kama vile kudhibiti idadi ya wabunge wanaohudhuria vikao vya bunge wakati mmoja