Habari

Corona yawaua Wakenya 18 ughaibuni

April 28th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA 18 ndio wamefariki ughaibuni kutokana na virusi vya corona, serikali imesema Jumanne.

Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Bw Macharia Kamau, alisema kuwa watu hao ni kati ya 85 walioambukizwa virusi katika nchi hizo.

Hata hivyo, 60 kati yao wamepona, huku mmoja akiwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) nchini Sweden.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, Bw Kamau alisema kuwa wengi kati ya waliofariki wanatoka katika maeneo ya New York na Boston nchini Amerika.

Wakati huo huo, imebainika kwamba Wakenya wanaoishi China walikataa kurejea nchini, licha ya serikali kuwaagiza kuwasilisha majina yao katika Ubalozi wa Kenya jijini Beijing ili kurejeshwa nchini.

Katibu huyo alisema ni Wakenya chini ya 200 waliofika kwenye ubalozi huo, idadi ambayo hata haiwezi kujaa kwenye ndege moja ya abiria.

“Tulijaribu tuwezavyo. Tuliwaagiza kujisajili ili kurahisisha kazi yetu kuwarejesha nyumbani. Hata hivyo, idadi iliyojisajili ni chache sana, kiasi kwamba tulilazimika kuahirisha safari yao hadi idadi inayohitajika itakapojaa,” akasema Bw Kamau.

Alieleza kuwa Wakenya hao sasa watarejeshwa nchini mnamo Mei 8, baada ya wengine 300 ambao wamekwama nchini India kurejeshwa mnamo Mei 4.

Aliitetea serikali dhidi ya kuwatelekeza Wakenya hao, licha ya masaibu waliyodai kupitia, akisema kuwa uchunguzi wao ulibaini kwamba ni Wakenya wachache tu waliojipata kwenye patashika hizo.

“Uchunguzi wetu ulibaini kuwa wale waliokuwa kwenye mzozo na Wachina ni raia wengi wa nchi za Afrika Magharibi kama Nigeria, ambapo walikuwa wakikataa kuzingatia kanuni zilizowekwa,” akasema.

Baadhi ya Wakenya hao walilalamika kudhulumiwa na mamlaka za China, huku wakimlaumu balozi wa Kenya nchini humo, Bi Sarah Serem, kwa kutowasaidia kwa vyovyote vile.

Kulingana takwimu za serikali, Wakenya wanaoishi ama kufanya kazi China ni kati ya 4,000 na 5,000.

China ni mojawapo ya nchi ambazo ni washirika wakuu wa kibiashara wa Kenya.