Habari

Corona yayumbisha utalii baada ya safari kusitishwa

March 13th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya Utalii wameingiwa na wasiwasi baada ya Kenya kuthibitisha kuwepo kwa COVID-19 nchini.

Sekta hiyo imeathiriwa baada ya wageni kukatiza ziara zao kuja Pwani kutokana na maradhi hayo na safari za ndege kusitishwa.

Ijumaa, Waziri wa Utalii Najib Balala alikiri kwamba sekta hiyo imeathiriwa pakubwa.

Utalii unatarajiwa kudorora zaidi baada ya serikali kuu kusitisha mikutano yote ya kimataifa iliyokuwa inatarajiwa mwezi huu wa Machi. Kwa sasa msimu huo ambao hauna wageni wengi unajikokota baada ya ugonjwa huo kusambaa katika zaidi ya nchi 115 duniani.

“Inasikitisha sana kwamba tumepata ugonjwa huu lakini tuna matumaini kwamba serikali itaweka mikakati kuzuia maambukizi zaidi. Ni dhahiri kuwa utalii utaathiriwa kwa sababu ya kusitishwa kwa safari za ndege. Lakini tunasalia na utalii wa barani Afrika na wale wa nchi jirani,” alisema Dkt Sam Ikwaye.

Kenya ni nchi ya 16 kuathiriwa na ugonjwa huu barani Afrika.

“Katika hoteli ya Pride Inn Paradise, Shanzu, nilikuwa natarajia kuwa na wageni wa kimataifa kwenye kongamano la 63 la wawekezaji wa viwanja vya ndege lakini warsha hiyo imesitishwa,” alisema mkurugenzi mkuu wa hoteli hiyo Hasnain Noorani.

Mkutano huo ulikuwa unatarajiwa kufanyika mnamo Machi 14 hadi 20.

Mkutano huo wa kimataifa ulikuwa uwalete pamoja zaidi ya wageni 400 ambao wengine walitarajia kukodi hoteli jirani ya Serena.

“Tunasihi muungano wa benki nchini kuwawia radhi wamiliki wa hoteli wenye madeni au mikopo wakati huu tunapopitia hali ngumu. Tulitarajia sekta hii ipigwe jeki na mikutano ya kimataifa lakini matumaini yetu yamedidimia kwa sababu ya ugonjwa huu,” alisihi Bw Noorani.