Habari Mseto

Corona yazindua Kenya usingizini, yazua ubunifu

April 12th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU 

LICHA ya kutishia maisha, jamii na uchumi wa nchi, virusi vya corona vimechochea vyuo, watu binafsi na kampuni kuwa bunifu katika kutafuta mbinu za kukabiliana na janga hili.

Hii imedhihirisha uwezo wa Wakenya kuwa wabunifu iwapo tu watapewa motisha wa kuvumbua teknolojia zinazoweza kusuluhisha matatizo ya kila siku, sio tu wakati wa majanga.

Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Nyeri: Kabla ya janga la corona kuzuka, chuo hiki cha teknolojia kilikuwa na kitengo cha kibiashara cha Dekut Enterprise Company, lakini hakikuwa kikifahamika.

Janga la corona lilipozuka, kitengo hiki kilipata kibali cha kutengeneza maski, sanitaiza na nguo maalum za kujikinga kuambukizwa magonjwa (PPE).

Utengenezaji wa bidhaa hizo unasukumwa na ubunifu wa Idara ya Kemia ya chuo hicho. Dkt Moses Ollengo alithibitisha kuwa aina ya sanitaiza wanayounda ina uwezo wa kuua viini vya corona.

Idara ya Uhandisi nayo inafanya majaribio ya kuunda vifaa vya kusaidia watu kupumua, ambavyo vimekuwa haba kote duniani tangu corona ilipozuka.

Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa: Chuo hiki tayari kimeunda kifaa cha kusaidia wagonjwa kupumua, ambacho wanakiita Flence Ventilator.

Uvumbuzi huo umeshirikisha mhadhiri wa uhandisi wa matibabu, wanafunzi wake 26 na wajuzi wengine watatu.

Wavumbuzi hao wakisimamiwa na mhandisi David Malombe walifanya kazi kwa siku sita mfululizo kukamilisha kifaa hicho, licha ya kukumbana na changamoto nyingi.

Fadscape Ventures: Bw Anthony Karanja na wenzake watatu walianzisha kampuni ya Fadscape Ventures kutengeneza vifaa vya kujikinga uso mzima.

Vijana 15 waliposikia kuhusu juhudi za Karanja na wenzake walijiunga nao katika kufanikisha wa ndoto yao. Kufikia sasa Fadscape Ventures wametengeneza vifaa maalum vya kufunika uso na PPEs.

Kitale Woolshop: Mkurugenzi wa maduka ya Kitale Woolshop John Njoroge, amejitwika jukumu la kutengeneza maski za bei nafuu kuwafaa wakazi wa Kaunti ya Trans-Nzoia.

Bw Njoroge anasema wanatengeneza maski 7,000 kila siku na kuziuza kwa Sh40 kwa moja. Anasema haja yake si faida bali kuwasaidia wakazi kujikinga wasiambukizwe corona.

Kiwanda cha Nguo cha Kaunti ya Kitui (Kicotec): Kabla ya kuzuka kwa corona, kiwanda hiki kilikuwa kikishona nguo hasa sare za maafisa wa serikali.

Lakini baada ya kufahamika kuna uhaba wa maski kutokana na mahitaji yake kila pembe ya dunia, kiwanda hiki sasa kinaangazia zaidi ushonaji maski na kinatengeneza 30,000 kwa siku.

Chuo Kikuu cha Kenyatta: Chuo hiki jana kilizindua sampuli ya mashine inayotumiwa kuwezesha wagonjwa kupumua. Kifaa hicho kilitengenezwa na idara ya matibabu katika chuo hicho kwa ushirikiano na wahandisi.

Kiwanda cha nguo cha Rift Valley (Rivatex): Kiwanda hiki kinachosimamiwa na Chuo Kikuu cha Eldoret, kimejitwika jukumu la kutengeneza barakoa ambazo ni muhimu katika vita dhidi ya virusi vya corona. Kinalenga kutengeneza barakoa 5,000 kwa siku.

Ripoti za Irene Mugo, Nicholas Komu, Diana Mutheu, Daniel Ogeta, Osborn Manyengo, Valentine Obara