Kimataifa

Coronavirus sasa yafika Afrika, Algeria yatangulia

February 26th, 2020 2 min read

NA MASHIRIKA

SERIKALI ya Algeria imethibitisha kisa cha kwanza nchini humo cha mwathiriwa wa maradhi ya homa ya Corona.

Waziri wa Afya wa Alger, Abdel Rahman Ben Bouzid alitangaza kupitia runinga ya serikali ya ENTV kuwa mwathiriwa ni raia wa Italia.

Mwathiriwa huyo aliwasili nchini humo mnamo Febrauri 17 na ametengwa kwa ajili ya matibabu.

Algeria ni nchi ya pili barani Afrika kuthibitisha kisa cha homa ya virusi vya Corona (Covid-19).

Misri ilikuwa ya kwanza kuthibitisha kisa cha mwathiriwa wa homa ya Corona lakini baadaye ikasema kuwa hakuwa na maradhi hayo hatari ambayo yameua zaidi ya watu 2,700 kote duniani.

Misri Jumatano ilisema kuwa shirika lake la ndege la Egyptair halitarejelea safari zake kuelekea nchini China.

Serikali ya Misri ilipiga marufuku ndege zake kwenda China mnamo Februari 1, mwaka huu, lakini ikasema kuwa ingerejelea safari zake kuanzia leo.

Lakini Jumatano ilisema kuwa marufuku hiyo itaendelea kwa muda usiojulikana.

Shirika la Afya Duniani (WHO) tayari limeonya kuwa mamilioni ya watu huenda wakaangamia iwapo maradhi ya homa ya Corona yatasambaa barani Afrika.

Korea Kusini Jumatano ilitangaza kuwa watu 11 tayari wameangamia huku wengine 1,146 wakiwa wanaendelea kutibiwa kutokana na maradhi hayo hatari.

Ufilipino jana ilipiga marufuku safari zote za kuelekea Korea Kaskazini kama njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwa homa hiyo.

Wakati huo huo, raia wa Iran wameanzisha kampeni inayojulikana kama “Tutashinda Virusi vya Corona” baada ya naibu waziri wa Afya Iraj Harirchi kupatikana na virusi vya ugonjwa huo.

Jumla ya watu 15 wamefariki nchini Iran kutokana na maradhi hayo huku wengine 95 wakiwa wanaendelea kutibiwa.

Iraj Harirchi alishikwa na kikohozi na kutokwa na jasho jingi alipokuwa akihutubia wanahabari jijini Tehran Jumatano na alipopimwa alipatikana na virusi vya Corona, kulingana na msemaji wa serikali Ali Rabiei.

Baada ya kufanyiwa vipimo, naibu waziri huyo alithibitisha kuwa anaugua homa ya Corona.

“Hata mimi nimeambukizwa homa ya Corona. Nimetengwa na ninafanyiwa matibabu,” akasema waziri huyo kupitia video aliyotia katika mitandao ya kijamii na kupeperushwa katika runinga ya serikali ya nchi hiyo.

Mbunge anayewakilisha jiji la Tehran, Mahmoud Sadeghi, pia alipatikana na virusi hivyo. Sadeghi kupitia ujumbe wake kwa Twitter aliitaka serikali ya nchi hiyo kuachilia huru wafungwa wa kisiasa ili wasije wakapatwa na virusi vya Corona.