Habari Mseto

COTU yapinga wafanyakazi kukatwa ada ya nyumba

June 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Muungano wa vyama vya wafanyikazi (COTU) umepinga pendekezo la Hazina ya Maendeleo ya Nyumba (NHDF).

Waziri wa Fedha Henry Rotich alipendekeza asilimia 0.5 ya mshahara kufadhili hazina hiyo katika bajeti ya 2018/2019.

Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli alisema pendekezo la marekebisho ya Kifungu cha 31, Sheria ya Ajira(2007) ili kupata ufadhili huo ni kinyume cha taratibu za kimataifa za Shirika la Leba (ILO) kuhusiana na mshahara.

Atwoli alisema hatua hiyo itaumiza wananchi ambao tayari wanaendelea kuumizwa na ushuru wa juu, zaidi ya kuwa gharama ya maisha imeendelea kuongezeka.

“Cotu inaunga mkono Shirikisho la Waajiri (FKE) kupinga pendekezo la marekebisho hayo,” alisema Bw Atwoli Ijumaa.

Ongezeko la ada zaidi kufadhili ajenda ya maendeleo ya rais litaathiri waajiri na pia waajiriwa, alisema Bw Atwoli.

Aliongeza kuwa ada kama hizo za kila mara kwa waajiri na wafanyikazi zitafukuza wawekezaji nchini.