Michezo

Coutinho afanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu

April 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Philippe Coutinho anayewaniwa pakubwa na Chelsea nchini Uingereza amefanyiwa upasuaji kwenye kifundo cha guu lake la kulia.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 sasa atasalia mkekani kwa kipindi cha takriban wiki sita kabla ya kuanza mazoezi mazito.

Wakitumia mtandao wao wa Twitter, Bayern ambao kwa wanajivunia huduma za Coutinho kwa mkopo kutoka Barcelona, wamethibitisha kwamba upasuaji huo ulikamilika vyema na salama.

“@Phil_Coutinho alifanyiwa upasuaji kwenye kifundo cha mguu wake wa kulia. Upasuaji ulikamilika vizuri na kwa sasa atasubiri kwa zaidi ya siku 14 kabla ya kuanza mazoezi mepesi. Huenda awe nje kwa hadi wiki sita kabla ya kuanza mazoezi. #Rejea kwa matao ya juu zaidi, Philippe!”

Mnamo Aprili 24, 2020, Countinho ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Liverpool, alionekana akiondoka katika kambi ya mazoezi ya Bayern akiwa na bandeji mguuni huku akitembea kwa usaidizi wa mikongojo.

Iwapo Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) itarejelewa Meo 9, 2020 jinsi ambavyo imeratibiwa, basi Coutinho hatakuwa sehemu ya kikosi cha Bayern ambao wanajivunia ukiritimba mkubwa katika historia ya soka ya Ujerumani.

Tangu aagane na Barcelona, Coutinho ameridhisha zaidi kambini mwa Bayern ambao kocha Hansi Flick amewataka sasa kumpokeza mkataba wa kudumu.

Hata hivyo, itawalazimu Bayern kuwapiga kumbo Chelsea na Juventus ambao wako radhi kufungulia mifereji yao ya fedha kwa minajili ya huduma za nyota huyo wa timu ya taifa ya Brazil.

Liverpool ambao walikuwa wakihusishwa na uwezekano wa kumsaini upya Countinho walijiondoa katika vita hivyo.

Nguli wa soka nchini Brazil, Rivaldo, amesema kwamba Coutinho ana uwezo wa kurejea katika ubora wake wa zamani iwapo ataingia katika sajili rasmi ya Chelsea badala ya kurejea Barcelona atakaoendelea kuishi katika kivuli cha nahodha Lionel Messi.

Hadi kufikia sasa muhula huu, Coutinho ambaye pia anaviziwa na Arsenal na Tottenham Hotspur amefungia Bayern mabao tisa na kuchangia mengine manane katika mechi 25 za Bundesliga.