Habari

COVID-19: 45 waliotangamana na mgonjwa wajulikana

March 14th, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

WATU 45 waliotangamana na mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa kuwa na virusi vya corona Kenya wamepatikana huku serikali ikiwahimiza Wakenya wawe mstari wa mbele katika juhudi za taifa kujiandaa kukabiliana na mkurupuko huo.

Kulingana na Wizara ya Afya, 22 miongoni mwao waliotagusana kwa karibu na mgonjwa huyo walikuwa wametengwa katika kituo maalum cha Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) katika Hospitali ya Mbagathi.

Aidha, watu 23, raia wa mataifa mbalimbali waliokuwa katika ndege moja na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 27 anayetibiwa katika KNH, pia walikuwa wamepatikana na kutakiwa kujitenga kwa muda wa siku 14.

Akihutubia vyombo vya habari Jumamosi, Afisa Mkuu katika Wizara ya Afya Dkt Mercy Mwangangi alieleza kwamba chembechembe kutoka kwa watu hao 22 zilikuwa zikifanyiwa vipimo katika Taasisi ya Uchunguzi Nchini (Kemri)

“Wizara ya Afya imewapata watu 22 waliotagusana kwa karibu na ambao wametengwa katika Kituo cha KNH katika Hospitali ya Mbagathi. Chembechembe za watu hawa kwa sasa zinafanyiwa vipimo katika Kemri,” alisema.

Akaongeza: Watu wengine 23 wa asili mbalimbali waliosafiri katika ndege moja na mgonjwa huyo pia wamepatikana na kushauriwa kujitenga kwa siku 14. Kitengo cha Dharura cha MOH kinawafuatilia hadi siku hizo 14 ziishe.

Msemaji wa serikali Kanali Cyrus Oguna alisema kwamba serikali ilikuwa imemakinika vilivyo huku akiwahimiza Wakenya kuzingatia viwango vya juu zaidi vya usafi katika kukabiliana na COVID-19.

“Maandalizi yetu yako katika upeo wa juu zaidi iwezekanavyo. Hatuwezi kufikia kiwango cha asilimia 100 ikiwa hatutahusisha mwananchi wa kawaida. Kila mwananchi ni sharti ajihusishe katika juhudi za kujikinga. Wakati umewadia kwetu kudumisha kiwango cha juu zaidi cha usafi ili kuchangia binafsi katika kiwango cha kujiandaa kwa taifa,” alisema Kanali Oguna.