Makala

COVID-19: Asimulia jinsi alivyofungiwa mashambani wakati akitarajia kurejea jijini Nairobi

May 18th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KILA mwanzoni mwa mwezi Michael Murimi ambaye ni mfanyakazi na mkazi katika Kaunti ya Nairobi, huzuru mashambani Karatina, Nyeri, alikozaliwa.

Kijiji cha Thunguri ndiko wazazi waliko na hufika huko ili kuwajulia hali.

Mapema Aprili 2020 kama ilivyo ada yake, Murimi alifunga safari kuelekea humo.

Ni mpishi wa hoteli ya Kifahari ya Chinese, Nairobi, na alipata ruhusa ya siku kadhaa.

Safari hiyo ilikuwa wiki kadhaa baada ya Kenya kutangazwa kuwa mwenyeji wa Covid-19, ambao sasa ni janga la kimataifa.

Aprili 6, 2020, kiongozi wa nchi Uhuru Kenyatta alitoa amri ya kutoingia na kutotoka kaunti ya Nairobi ili kudhibiti msambao wa Covid – 19, wakati huo visa vya maambukizi vikiwa 158.

Kaunti zingine zilizoathirika na amri hiyo ni pamoja na Mombasa, Kilifi na Kwale.

“Nilipaswa kurejea mnamo Aprili 8, 2020, ila mpango huo ulisambaratika kufuatia amri ya Rais,” Murimi akaambia Taifa Leo.

Licha ya kuwasilisha ombi lake kurejea kazini, katika idara husika, Murimi amesema jitihada hizo zimegonga mwamba.

Ni baba wa watoto watatu na familia yake ipo jijini Nairobi, ambapo anasema wanahangaika kupata mahitaji ya kimsingi.

“Mwishoni mwa mwezi kodi ya nyumba inasubiriwa kulipwa. Ombi langu lisipokubalika, mambo yataendelea kuwa magumu kwa familia yangu,” akasema. Isitoshe, hajajua hatma ya nafasi yake kazini.

Hali iliyomfika Murimi inaonyesha taswira ya maelfu ya Wakenya wengine waliofungiwa nje ya kaunti wanazofanyia kazi.

Mnamo Jumamosi, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuongezwa muda zaidi – siku 21 – wa amri ya kutoingia na kutotoka kaunti zilizoorodheshwa. Hiyo ina maana kuwa amri hiyo itadumu hadi Juni 6.

Aidha, amri hiyo ilitolewa ili kudhibiti usambaaji wa virusi vya corona katika kaunti zilizotajwa, kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi.

Michael Murimi anasema kwa sasa anajishughulisha na shughuli za kilimo, ili kusukuma gurudumu la maisha. Kufikia sasa Kenya ina zaidi ya visa 800 vya maambukizi ya Covid – 19, huku serikali ikiendelea kuweka mikakati zaidi kuzuia msambao wa virusi vya corona.