Makala

COVID-19: Baadhi ya waishio katika nyumba za kulipia kodi wajipata pabaya

April 30th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BI Charity Wanjiru ni mmoja wa wafanyakazi walioathirika Machi 2020 baada ya serikali kuagiza mikahawa ifungwe ili kusaidia kuzuia usambaaji wa Covid-19.

Licha ya Wizara ya Afya mapema wiki hii kuruhusu mikahawa ifunguliwe tena ingawa kwa masharti, Wanjiru ambaye ni mhudumu wa mkahawa mmoja eneo la Engen, Kahawa, Kiambu, ameketi akitafakari jinsi atakavyomudu kulipa kodi ya nyumba.

Mama huyo wa watoto wawili wa umri wa miaka sita na 13 anasema ana deni la kodi ya mwezi huu wa Aprili ambao unakamilika leo Alhamisi, kwa kuwa mwezi Machi alilipwa nusu ya mshahara wa kawaida.

“Tulilipwa siku tulizofanya kazi pekee, mapato niliyopokea yakawa ya kulisha familia yangu,” anaeleza.

Licha ya afueni mikahawa kufunguliwa, anaiambia ‘Taifa Leo’ kuwa masharti yaliyowekwa na serikali yamewazuia kurejea kazini.

“Maagizo yaliyotolewa yanahitaji gharama ya juu kuyaafikia ihali hatujakuwa kazini na hivyo hatuna pesa,” akalalamika.

Kabla mkahawa kuruhusiwa kuhudumu, wafanyakazi wote wanapaswa kupimwa ikiwa wana virusi vya corona, mikahawa pia ikitakiwa kutafuta upya leseni ili kuhakikisha inazingatia taratibu na masharti kuzuia maambukizi.

Ni masharti yanayoonekana kulemea wawekezaji katika sekta hiyo. Wanjiru anasema landilodi amekuwa akimbishia mlango, mwezi Mei ukibisha hodi, asijue hatua atakayochukuliwa.

Mpangaji huyo ni mmoja wa wengi wanaoendelea kuhangaika kufuatia athari za Covid-19 katika biashara.\

“Mambo yanaendelea kuwa magumu, maajenti ya kupangisha nyumba za kukodi na malandilodi huwataelewa wengine wetu tulisimamishwa kazi. Pesa tulizonazo kwa sasa ni za kulisha familia,” broka wa kuuza vipande vya ardhi Bw Charles Mwangi anasema, akibainisha biashara hiyo imeathirika kwa kiasi kikubwa.

Visa vya malandilodi kufurusha walio na deni la kodi na hata kuwang’olea mapaa ya nyumba, vimeripotiwa.

Kulingana na wapangaji tuliozungumza nao, licha ya serikali kupambana kudhibiti maambukizi ya Covid-19, inapaswa kuibuka na mikakati kuwapa afueni Wakenya wengi wanaokodi nyumba na wasio na uwezo kifedha.

Malandilodi wachache mno wamefuta kodi za wapangaji wao kwa muda wa miezi kadhaa ijayo, kufuatia athari za corona.

Wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alisema hana uwezo kisheria kuamuru wamiliki wa nyumba za kupangisha kuondoa kodi au kuipunguza.

“Tumefunzwa kuwa na utu, ninachowaomba ni tuwe na ubinadamu wakati huu mgumu,” Rais akawahimiza, wakati akihojiwa na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa Kiswahili.

Virusi vya corona vimekuwa kero kuu ulimwenguni kote ambapo vinaendelea kusambaratisha uchumi wa mataifa, kusababisha biashara, kampuni na masharika kufungwa.

Watu wamepoteza nafasi za kazi na baadhi ya wanaoendelea kuhudumu mishahara yao kupunguzwa.