Habari

COVID-19: Bunge laahirisha vikao vyake hadi Aprili 14

March 18th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa limeahirisha vikao vyake hadi Aprili 14 kutokana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona mbayo yamekwamisha shughuli katika sekta za umma na zile binafsi.

Hoja ya kusitishwa kwa shughuli za bunge iliwasilishwa katika kikao cha alasiri mnamo Jumanne na kiongozi wa wengi Aden Duale, saa chache baada ya Kenya kuthibitisha kisa cha nne cha ugonjwa huo hatari nchini.

Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini alisema hiyo ni mojawapo ya hatua ambazo asasi ya bunge imechukua kuzuia kuenea kwa virusi vinavyosababisha COVID-19.

Parliament adjourned sittings on the day the country confirmed its fourth case of coronavirus.

“Kwa kuzingatia kuwa ugonjwa huu, ambao kufikia sasa haujapata tiba, umesambaa katika mataifa mengi. Na kwa sababu kuna uwezekano kwamba utaathiri idadi ya watu duniani, bunge hili linaamua kuahirisha vikao vyake kuanzia Jumatano Machi 18, 2020, hadi Jumanne Aprili 14, 2020, saa nane na nusu alasiri,” akasema Duale akiwasilisha rasmi hoja hiyo.

Bw Duale alisema bunge la kitaifa limelazimika kuchukua hatua hiyo licha ya kwamba kuna kalenda yake rasmi.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini alipendekeza kuwa serikali ibuni hazina maalum ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ambao wataathiriwa kutokana na kusitishwa kwa shughuli katika sekta mbalimbali za uchumi.

“Biashara nyingi zitaathirika; hasa zile ndogo. Kwa hivyo, bunge hili linafaa kubuni hazina maalum ambayo itawasaidia wafanyabiashara wetu kujiinua kibiashara,” Duale akasema.

Kiongozi wa wachache katika bunge hilo John Mbadi aliunga mkono kauli ya Bw Duale na akaitaka Wizara ya Fedha kukadiria athari za mkurupuko wa ugonjwa wa COVID-19 kwa uchumi wa taifa, akisema biashara nyingi zitaathirika pakubwa.

Bw Duale alisema Tume ya Huduma za Bunge (PSC) itaweka mipango ambayo itawezesha bunge lifidie muda ambao litakuwa limepoteza wakati ambapo limesitisha shughuli kutokana na dharura hii ya kiafya.

“Vilevile, tumekubaliana kwamba katika kipindi hiki Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi atakuwa huru kuwasilisha majina ya watu walioteuliwa kwa nyadhifa kuu serikalini kwa kamati husika bila kuita kikao cha bunge lote,” akaongeza.