Michezo

COVID-19: Cavani kusubiri zaidi kabla ya kuchezea Manchester United

October 7th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

SAJILI mpya wa Manchester United, Edinson Cavani, atachelewa zaidi kuwajibishwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa sababu ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Sogora huyo raia wa Uruguay alikamilisha uhamisho wake hadi Man-United mnamo Oktoba 6, 2020 baada ya kutokea Ufaransa alikokuwa akiishi tangu mkataba wake na Paris Saint-Germain (PSG) ukatike mnamo Juni 2020.

Ina maana kwamba Cavani, 33, atalazimika kutiwa karantini kwa kipindi cha siku 14 kuanzia siku alipotua ugani Old Trafford, Uingereza kurasimisha uhamisho wake hadi kambini mwa Man-United.

Mchuano ujao wa Man-United katika EPL ni gozi litakalowakutanisha na Newcastle United mnamo Oktoba 17, 2020 uwanjani St James’ Park.

Kwa kuwa Cavani hatakuwa amekamilisha kipindi cha siku 14 za karantini kufikia wakati huo, Solskjaer atakosa huduma za nyota huyo wa zamani wa Napoli. Man-United hawatakuwa pia na fowadi chipukizi Anthony Martial ambaye kwa sasa anatumikia marufuku.

Martial ambaye ni raia wa Ufaransa, alionyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumzaba kofi fowadi Erik Lamela wa Tottenham Hotspur wakati wa mechi ya EPL iliyowakutanisha ugani Old Trafford mnamo Oktoba 4, 2020. Spurs waliibuka na ushindi mnono wa 6-1 kwenye mechi hiyo.

Cavani ambaye pia hatapata fursa ya kushiriki mazoezi ya pamoja na wachezaji wengine wa Man-United, atakosa pia gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) litakalowakutanisha Man-United na PSG mnamo Oktoba 20, 2020 uwanjani Parc des Princes, Ufaransa.

Man-United wametiwa katika Kundi H kwa pamoja na PSG, RB Leipzig na Istanbul Basaksehir kwenye hatua ya makundi ya kipute cha UEFA msimu huu wa 2020-21.

Fowadi na nahodha wa Spurs na timu ya taifa ya Uingereza, Harry Kane alilazimika pia kuingia karantini kwa siku 14 baada ya kurejea Uingereza kutoka Barbados alikokuwa kwa likizo mnamo Agosti, 2020.