Covid-19: Fainali za Copa America nchini Brazil kuendelea jinsi zilivyopangwa licha ya pingamizi

Covid-19: Fainali za Copa America nchini Brazil kuendelea jinsi zilivyopangwa licha ya pingamizi

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

FAINALI za Copa America zilizoratibiwa kuanza Juni 13, 2021 nchini Brazil, zitaendeleza jinsi zilivyopangwa baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kuamua hivyo.

Mnamo Juni 10, 2021, majaji wa Mahakama ya Juu nchini Brazil walitupilia mbali maombi ya waliyokuwa yamewasilisha kortini kuzuia fainali za kipute hicho kuandaliwa nchini humo kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa mujibu wa malalamishi, ilihojiwa kwamba maelfu ya maisha ya wakazi wa Brazil yalikuwa katika hatari iwapo fainali za Copa America zingeandaliwa nchini humo.Hata hivyo, majaji walishikilia kwamba Katiba ya Brazil haina uwezo wa kuipa korti mamlaka ya kuzuia kuandaliwa kwa kivumbi hicho cha Copa America.

Badala yake, walitaka magavana na mameya wa miji mikuu kukaza kanuni za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona katika himaya zao.Aidha, walikiri kushangazwa na maamuzi ya dakika za mwisho za Rais Jair Bolsonaro kuidinisha kipute hicho kufanyika Brazil bila mahudhurio ya mashabiki.

Vikosi vitakavyoshiriki Copa America vitakuwa vikifanyiwa vipimo vya corona kila baada ya saa 48 huku wachezaji na maafisa wa vikosi vyao wakinyimwa uhuru wa kutembea ovyo. Vikosi vyote vinatarajiwa kuwasili katika majiji ambamo kipute hicho kitaandaliwa kwa kutumia ndege za kibinafsi.

Mashindano ya Copa America yaliyokuwa yafanyika mnamo 2020, yaliahirishwa kwa sababu ya corona na yalikuwa yaandaliwe kwa pamoja na Colombia na Argentina.Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) liliondoa fainali za kivumbi hicho nchini Argentina kwa sababu ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

“Conmebol inashukuru Shirikisho la Soka la Brazil kukubali kuwa wenyeji wa kipute hiki cha Copa America kati ya Juni 13 na Julai 10. Amerika Kusini sasa iko tayari kung’aa nchini Brazil,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Conmebol.

Awali, Argentina ilikuwa ishirikiane na Colombia kuandaa fainali za Copa America mwaka huu. Hata hivyo, Colombia walipokonywa idhini hiyo mnamo Mei 20 baada ya kuongezeka kwa visa vya maandamano yaliyochangiwa na hatua ya serikali kuongeza ushuru unaotozwa kwa bidhaa muhimu.

Mnamo Mei 22, serikali ya Argentina ilipiga marufuku safari zote za kuingia na kutoka nchini humo baada ya visa vipya 35,000 vya maambukizi ya corona kuripotiwa siku hiyo.Kwa upande wao, maandamano ya kulalamikia jinsi janga la corona linavyoshughulikiwa na serikali ya Brazil chini ya Rais Jair Bolsonaro yalifanyika mnamo Mei 29, 2021.

Brazil ambayo imesajili takriban vifo 475,000 kutokana na corona ndiyo nchi ya pili baada ya Amerika ambayo imeathiriwa zaidi na janga hilo duniani.Brazil ndio mabingwa watetezi wa Copa America baada ya kutia kapuni taji hilo mnamo 2019.

  • Tags

You can share this post!

Dortmund wakataa ofa ya Sh9.4 bilioni ambazo Man-United...

Pigo tena kwa Uhuru korti ikibatilisha amri