Habari Mseto

COVID-19: Idadi jumla ya vifo nchini Kenya yafika 1,452

November 30th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

IDADI ya watu waliofariki kutokana na Covid-19 Jumapili ilipanda hadi kufika 1,452 baada ya wagonjwa saba zaidi kufariki kutokana na ugonjwa huo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema idadi jumla ya visa vya maambukizi nchini kufikia Jumapili ilitimu 83,316 baada ya watu wenginee 711 kupatikana na virusi vya corona.

“Watu wengine 711 wamethibitishwa kuwa na Covid-19 baada ya sampuli 6,672 kupimwa ndani ya saa 24. Idadi jumla ya sampuli zilizopimwa sasa imefika jumla 885,933,” Bw Kagwe akasema.

Kwa mara nyingine Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa visa vipya vya maambukizi kwa kuandikisha visa vipya 190 katika ya visa hivyo vipya 711.

Inafuatwa na Mombasa yenye visa 88, Nakuru (78), Nyandarua (35); Murang’a (34); Kitui (30); Machakos (28); Nyeri (27); na Embu (25).

Kaunti ya Busia nayo ina visa vya 21; Kiambu (17); Vihiga (16); Kisumu (13); Kilifi (11); Isiolo (11), Meru (10); Turkana (10); Kirinyaga (9); Bungoma (9); Laikipia (8); Kakamega (7); Kajiado (6); Kwale (5); Homa Bay (5); Makueni (4); Kisii (2); Uasin Gishu (2) na Migori (2);

Nazo kaunti za Nandi, Samburu, Kericho, Tharaka Nithi, Baringo, Taita Taveta, Lamu na Bomet ziliandikisha kisa kimoja kila moja.

Habari njema ni kwamba jumla ya wagonjwa 576 Jumapili walithibitishwa kupona na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida. 469 kati yao walikuwa wakihudumu chini ya mpango wa utunzaji nyumbani ilhali 107 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali.

Jumla ya wagonjwa 1,262 nao wangali wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku wengine 7, 806 wakiuguzwa chini ya mpango wa utunzaji nyumbani.

“Wagonjwa 68 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU), 42 wanasaidiwa kupumua kwa kutumia mitambo ya “ventilators” ilhali 24 wanaongezewa hewa ya oksijeni,” akasema Waziri Kagwe.