Habari

COVID-19: Idadi jumla ya visa nchini Kenya sasa ni 1,192

May 23rd, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

WATU wengine 31 wamepatikana kuwa na virusi vya corona baada ya matokeo ya sampuli zilizofanyiwa vipimo kipindi cha saa 24 zilizopita kufanyiwa kuwa tayari, ametangaza Rais Uhuru Kenyatta.

Sasa idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini imefikia 1,192.

Akihutubia taifa kupitia taarifa iliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Ikulu ya Nairobi Jumamosi, Rais Kenyatta ametangaza kwamba jumla ya watu 57, 650 wamefanyiwa vipimo kufikia sasa.

“Tumepima sampuli 57,650 ambapo miongoni mwake, watu 1,192 wamepatikana kuwa na Covid-19. Wakati huohuo tumepoteza Wakenya wenzetu 50 ambao wamefariki kutokana na ugonjwa huu,” amesema kiongozi wa nchi.

Pia ameeleza kwamba serikali imekuwa ikisambaza jumla ya Sh250 milioni kwa lengo la kusaidia familia maskini kutokana na athari za janga la virusi vya corona nchini.

“Kuna Wakenya wengi ambao wameshushwa hadhi yao kiasi kwamba hawawezi kulisha familia zao wala kulipa kodi za nyumba na ndiposa kila wiki serikali imekuwa ikisambaza kiasi cha Sh250 milioni kwa familia zilizoathirika zaidi,” amesema.

Akifafanua hatua ya serikali ya kutuma hela moja kwa moja kielektroniki kwa familia zisizojiweza badala ya mtindo wa zamani wa kutoa msaada wa vyakula kwa makundi hayo, Kenyatta amesema serikali imenuiwa kuwapiga teke mawakala na wakati uo huo kuimarisha uchumi.

“Hapo awali tulikuwa tukiharakisha kutoa msaada wa chakula kwa wahasiriwa wa majanga. Tulichogundua baada ya muda ni kwamba tulipoteza karibu nusu ya raslimali hizo kwa maajenti na waandalizi. Ni kiasi kidogo mno kilichofikia waathiriwa,” ameeleza.

Wakati huo huo, kiongozi wa nchi amewahimiza Wakenya kuzingatia masharti ya Wizara ya Afya akionya kuwa kukosa kufanya hivyo kutasababisha idadi ya maambukizi ya Covid-19 nchini kuzidi kuongezeka.

“Ni matumaini yangu kwamba tutaona visa vya maambukizi vikipungua kwa sababu nina imani Wakenya watazingatia masharti. Ni sharti tufahamu kila wakati kwamba kuna uwezekano wa visa hivyo kuongezeka ikiwa hatutafanya kinachohitahika,” akasema.