Habari

COVID-19: Idadi jumla yagonga visa 2,989

June 9th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WATU 127 zaidi wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona, idadi jumla ya wagonjwa wa Covid-19 waliothibitishwa nchini ikifika 2,989

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman amesema Jumanne visa hivyo vimethibitishwa kutoka kwa sampuli 2,247 zilizokaguliwa na kufanyiwa vipimo katika kipindi cha muda wa saa 24 zilizopita.

Kati ya maambukizi hayo, 124 ni Wakenya na watatu ni raia wa kigeni.

“Leo tumekaribia kufikisha visa 3,000. Kulingana na watafiti, hali hii inatokana na ongezeko la maambukizi maeneo tofauti nchini,” Dkt Aman akaambia wanahabari katika Afya House, Nairobi.

Katika visa hivyo vipya, mgonjwa wa umri wa chini ni mtoto mwenye umri wa wiki tatu, huku  umri wa juu ukiwa ni miaka 72.

Nairobi na Mombasa zinaongoza katika maambukizi, zikisajili visa vipya 62 na 34 kila moja.

Aidha, Busia imekuwa na wagonjwa 14, Machakos, Kilifi na Kiambu zikiwa na visa vinne kila kaunti.

Kaunti za Kwale na Uasin Gishu zimekuwa na mgonjwa mmoja kila moja.

Katika kipindi cha saa 24, wagonjwa 24 wametangazwa kupona idadi ya waliopona nchini ikifika 873.

Nayo idadi ya waliofariki kutokana na Covid-19 imegonga 88 baada ya wagonjwa watatu zaidi kufariki.

Visa vya unyanyapaa kwa waliopatikana na ugonjwa huu ambao sasa ni kero ya kimataifa vinaendelea kuripotiwa, na akikashifu matendo ya aina hiyo, Dkt Aman amesema hayatapewa fursa kamwe akitaja kwamba yanahatarisha maisha ya waathiriwa.