Habari Mseto

COVID-19: Idadi ya visa vipya na vifo yarudi chini kiasi Jumatatu

December 7th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA Jumatatu kwa mara ya kwanza imeandikisha idadi ndogo ya vifo na visa vipya vya Covid-19 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Ni watu 199 waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona ndani ya kipindi cha saa 24 baada ya sampuli kutoka kwa watu 2,416 kupimwa.

Na watu watano zaidi walifariki kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha 1,531 idadi jumla ya wagonjwa ambao wamefariki kutokana na ugonjwa huo kufikia Jumatatu.

Kulingana na taarifa kutoka Wizara ya Afya, visa hivyo vipya 199 vinafikisha 88,579 idadi jumla ya visa vya maambukizi nchini tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kilipothibitishwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

Hii ni baada ya sampuli 934,215 kupimwa tangu wakati huo.

Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa visa vipya vya maambukizi kwa kuandikisha visa 77 vipya.

Mombasa ni ya pili kwa kuandikisha visa 21, Busia (20), Uasin Gishu (19), Meru (11), Kiambu (9), West Pokot (7), Kilifi (7), Turkana (5), Laikipia (4), Narok (4), Kajiado (4), Murang’a (3) na Kakamega (2),

Na kaunti za Nakuru, Kisumu, Embu, Machakos, Siaya na Kwale, zilisajili kisa kimoja kila moja.

“Habari njema ni kwamba jumla ya wagonjwa 485 wamepona na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida. Wagonjwa 416 walikuwa wakitunzwa nyumbani ilhali 69 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali,” akasema Waziri wa Afya Mutahi Kagwe katika taarifa hiyo.