Habari Mseto

COVID-19: Idadi ya visa vya maambukizi yazidi kuwa ya juu

October 22nd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

IDADI ya watu waliofariki kutokana na Covid-19 imepanda hadi 858 baada ya wagonjwa 16 zaidi kufikia Jumatano, Wizara ya Afya ilipotoa taarifa kuhusu ugonjwa huo nchini Kenya.

Kwenye ripoti kuhusu hali ya janga hilo iliyotolewa na wizara hiyo, visa 497 vya maambukizi ya corona vilithibitishwa katika kipindi hicho na kufikisha idadi jumla ya maambukizi nchini kuwa 46,144.

Wagonjwa hawa wapya walipatikana na virusi vya corona kutokana na sampuli 4,888 zilizopimwa ndani ya muda wa saa 24.

Kufikia Jumatano idadi jumla ya sampuli ambazo zimepimwa tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kigunduliwe nchini mnamo Machi 13, 2020, ni 632,669.

Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya wagonjwa ambao wanaongezewa hewa ya oksijeni katika vyumba vya kuwatunza wagonjwa mahututi (ICU) ilipanda hadi 41.

Wakati huo huo wagonjwa 238 wamepona na kuruhusiwa kuendelea na maisha yao ya kawaida japo watahitajika kuzingatia masharti ya kuzuia kuenea kwa corona. Kwa hivyo, idadi jumla ya waliopona imefika 32,760 tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa nchini.

Kwa ujumla watu 1,189 wakati huu wamelazwa katika hospitali mbalimbali huku wagonjwa 2,661 wakiuguzwa chini ya mpango wa utunzaji nyumbani.

Idadi ya maambukizi mapya yamethibitishwa katika kaunti zifuatazo; Nairobi imeandikisha visa vipya 227,Machakos (64), Mombasa (51), Uasin Gishu (37), Laikipia (28), Busia (19), Kajiado (11), Embu (10) , Nakuru (9), Wajir (7) huku kaunti za Kiambu na Kilifi zikiripoti visa sita kila moja.

Vile vile Kisumu ilikuwa na visa vine vipya sawa na Nyeri, Makueni (3), huku kaunti za Elgeiyo Marakwet, Meru, Kisii, na Turkana zikiandisha visa viwili kila moja. Narok, Homa Bay na Kakamega kila moja ziliandikisha kisa kimoja.