Michezo

Covid-19 imechelewesha azma yangu, haijaifuta – Conseslus Kipruto

August 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Olimpiki katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji, Conseslus Kipruto, amesema kwamba azma yake ya kuvunja rekodi ya dunia katika fani hiyo bado ingalipo licha ya ndoto hiyo kucheleweshwa na tukio la yeye kuugua Covid-19.

Kipruto almaarufu ‘Conse’, alitazamia kutumia duru ya kwanza ya mbio za Wanda Diamond League msimu huu jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14, 2020 kuvunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Hata hivyo, vipimo vya afya alivyofanyiwa vilibainisha kwamba ana virusi vya corona na hivyo azma yake ya kutikisa dunia nchini Ufaransa ikazimika ghafla.

Conse ametamalaki mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji katika miaka ya hivi karibuni na cha pekee anachokitamani zaidi kutokana na mbio hizo ni rekodi ya dunia.

“Corona haitavunja azma yangu. Kuendea rekodi ya dunia ni jambo ambalo nimekuwa nilipangia kwa muda mrefu. Rekodi hii imekuwa nje ya Kenya kwa kipindi kirefu mno. Kwa kuwa mimi ndiye bingwa wa dunia na Olimpiki katika mbio hizi, nahisi kwamba nina wajibu wa kufanya jambo na nilipania sana kutamba jijini Monaco kwa sababu nilikuwa katika fomu ya kuridhisha sana,” akasema.

Rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji iliwekwa na Mkenya raia wa Qatar Saif Saaeed Shaheen, awali akiitwa Stephen Cherono, mnamo 2004 jijini Brussels, Ubelgiji. Nyota huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 37, aliandikisha rekodi ya muda wa dakika 7:53.63.

Ni Mkenya Brimin Kipruto ambaye ni bingwa wa zamani wa Olimpiki katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, ndiye aliyewahi kukaribia kuvunja rekodi ya Shaheen alipokamilisha mbio hizo kwa muda wa dakika 7:53.64 mnamo 2011.

Muda bora zaidi wa Conse katika mbio hizo ni dakika 8:01.35. Aliandikisha muda huo mwaka jana alipojizolea medali ya dhahabu katika Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar.

Kipruto alitazamiwa kunogesha kivumbi cha Diamond League jijini Monaco mnamo Ijumaa ya Agosti 14 kwa kutoana jasho na Wakenya wenzake Abraham Kibiwott na Vincent Kipchumba.