Habari Mseto

COVID-19: Kamishna asisitizia wakazi haja ya kutoruhusu wageni kaunti ya Kwale

May 14th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

KAMISHNA wa Kaunti ya Kwale Bw Karuku Ngumo amewaomba wazee wa mtaa na wale wa mpango wa Nyumba Kumi wawe macho kuhakikisha wageni hawaingii katika kaunti hiyo kipindi hiki ambapo kila eneo linakabiliana na janga la corona.

Akizungumza na Taifa Leo Bw Ngumo amesema kuna baadhi ya watu ambao wanaingia katika kaunti hiyo kutoka nchi jirani ya Tanzania na kaunti jirani hatua anazotaja kama zinazotishia kuongeza idadi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Aidha amewataka wakazi kutowakaribisha wageni majumbani mwao, hadi pale janga la corona litakapodhibitiwa kisawasawa nchini.

“Hatuwakatazi kuwa wakarimu lakini tunachowaomba ni muwe macho wakati huu ambapo serikali iko katika mikakati ya kuangamiza janga la corona. Hata kama ni jamaa kutoka familia yako, usimkaribishe kwa sababu huwezi ukajua kama ameambukizwa virusi hivyo kisha akakuletea,” akasema.

Kufikia jana Jumatano idadi ya maambukizi nchini ilikuwa imefikia 737 huku watu 40 wakifariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Bw Ngumo aidha amewasihi wakazi wazingatie kanuni za usafi ili kujikinga wasiambukizwe ugonjwa huo.

“Hakikishine mnanawa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji na sabuni na ni bora zaidi muepuke kutembeleana muda huu. Tubaki nyumbani tutumie simu kusalimiana,” akasema.

Amewashajiisha wakazi wafanye kulihali kujilinda ikizingatiwa kwamba kaunti hiyo ina visa vichache vya ugonjwa huo.