Habari

COVID-19: Serikali yadokeza huenda ikaweka masharti makali

May 5th, 2020 2 min read

 

SYLVANIA AMBANI na CHARLES WASONGA

SERIKALI inatarajiwa kutangaza masharti mapya wakati wowote wiki hii, ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19 katika jamii.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema Jumanne taifa lingali linapambana kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona huku akiwalaumu baadhi ya Wakenya ambao wanakiuka masharti ya kudhibiti hali hiyo kimakusudi.

“Hatua zitachukuliwa dhidi ya wale ambao wanahujumu vita dhidi ya janga hili. Wao ndio wanachangia kupanda kwa idadi ya visa vya maambukizi. Hatima yetu kama wananchi itaamuliwa na jinsi tunavyotekeleza mikakati ya kuzuia maambukizi ya virusi hivi. Tunaweza kufikia lengo hili,” akasema Bw Kagwe jijini Nairobi alipotoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya janga hilo nchini.

Na alitangaza kuwa jumla ya watu 45 waliambukizwa virusi hivyo ndani ya saa 24 zilizopita huku mtaa wa Eastleigh ukiandikisha maambukizi 29.

Idadi hii inafikisha jumla ya maambukizi 535 nchini tangu kisa cha kwanza kilipogundulika mnamo Machi 13, 2020.

Waziri Kagwe aliwataka wale ambao wanaweza kufanya kazi wakiwa nyumbani wafanye hivyo, kwani hiyo ndiyo mojawapo ya njia za kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Vilevile, alielezea hofu kuhusu ongezeko la msongamano wa watu katikati mwa jiji la Nairobi licha ya serikali kuwataka watu kukaa nyumbani, isipokuwa wale wanaotoa huduma muhimu.

“Mwenendo wa watu kujumuika pamoja, watu kuketi pamoja wakati huu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kushiriki vinywaji mikahawani ni hatari. Hali inakuwa mbaya na huenda visa vya maambukizi vikapanda hadi 50 kila siku ikiwa watu hawatabadili mienendo yao,” Bw Kagwe akaonya.

Baadhi ya masharti ambaye yamewekwa na serikali kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona ni kafyu ya kuanza saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri na kusitishwa kwa watu kuingia au kuondoka kaunti zenye idadi ya juu ya maambukizi kama vile Kilifi, Kwale, Mombasa na Nairobi.

Vilevile, serikali imeamuru kufungwa kwa baa na vilabu vya burudani na vyumba vya ibada kama makanisa na misikiti.

Hata hivyo, wiki jana, serikali iliruhusu kufunguliwa kwa mikahawa na hoteli japo kwa masharti makali ya kuhakikisha kuwa wateja hawasambazi virusi vya corona.

Hatua hiyo ilichukuliwa kwa lengo la kutoa nafuu kwa wamiliki wa biashara hizo na wafanyakazi wao ambao wameathirika vikali baada ya amri ya kufungwa kwa biashara hizo kuanza kutekelezwa.