Habari

COVID-19: Kenya yarekodi idadi ya juu zaidi ya visa vipya kipindi cha saa 24

May 27th, 2020 1 min read

MAGDALENE WANJA na SAMMY WAWERU

KENYA imerekodi idadi kubwa zaidi ya visa vipya vya Covid-19 kuwahi kutangazwa katika kipindi cha saa 24 baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuthibitisha Jumatano kwamba kutoka kwa sampuli 3,077 kuna wagonjwa 123.

Kenya sasa ina jumla ya visa 1,471 vya Covid-19 tangu cha kwanza nchini kuripotiwa Machi 13, 2020.

Akiwahutubia wanahabari katika makao makuu ya wizara, Kagwe amesema kuwa Nairobi inaongoza ikiwa na visa 85 huku Kaunti ya Mombasa ikifuatia kwa visa 24 nazo Kajiado na Kisumu pia zikiwa na wagonjwa.

“Inasikitisha kuwa tumewapoteza watu watatu zaidi kutokana na ugonjwa huu. Watu hao walikuwa na maradhi mengine ambayo yalichangia katika vifo hivyo,” alisema Bw Kagwe.

Hii inafikisha 55 idadi ya waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchini.

Waziri Kagwe amesikitika kwamba baadhi ya wahudumu katika sekta ya uchukuzi tayari wamerejelea tabia na mienendo mibovu na ya kutojali ya hapo awali na kuwa hawazingatii sheria zilizowekwa za kuzuia maambukizi.

Waziri pia amezungumzia uozo katika wizara yake.

Amesema kuna visa kadhaa vya maafisa wanaoshiriki sakata za ufisadi.

Akieleza jinsi wanavyoshiriki ufisadi kupitia utoaji tenda au kandarasi katika idara, waziri ameonya kuwa siku zao zimewadia na kwamba asasi kama Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI), zinafanya uchunguzi.

“Hapa Afya House si ajabu kuona baadhi ya maafisa waliohudumu zaidi ya miaka 12 ikawa wamehamishwa ila wanaendelea kusalia papa hapa. Jiulize ni kwa nini hawataki kutoka?” Bw Kagwe akahoji.

Wizara hiyo imekuwa ikilaumiwa kwa visa vya ufisadi na matumizi mabaya ya raslimali za umma, huku vituo vya afya vya umma nchini vikitoa huduma duni.

“Sawa na sekta zingine, katika yetu pia tuna changamoto za ufisadi; hatukatai. Kuna maafisa wachache wanaoturudisha nyuma,” Bw Kagwe akaeleza.

Mwaka 2019 operesheni ya kukamata maafisa wakuu serikalini waliotuhumiwa kuhusishwa na visa vya ufisadi, ufujaji wa raslimali za umma na matumizi mabaya ya ofisi ilitekelezwa.