Habari

COVID-19: Kenya yathibitisha visa 688 vipya ikiwa idadi ya juu zaidi kwa siku

July 18th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA imeandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya Covid-19 Jumamosi ambapo jumla ya watu 688 wamepatikana na ugonjwa huo, hivyo kufikisha 12,750 idadi jumla ya maambukizi kuwahi kuripotiwa nchini tangu kisa cha kwanza Machi 13, 2020.

Wagonjwa hao walipatikana baada ya sampuli 4,522 kufanyiwa uchunguzi ndani ya muda wa saa 24 na hivyo kufikisha 238,168 idadi jumla ya sampuli zilizopimwa.

Miongoni mwa wagonjwa hao wapya 425 ni wanaume huku 263 wakiwa jinsia ya kike na hivyo kudumisha mwenendo wa wanaume wengi kuambukizwa kuliko wanawake.

Mwathiriwa mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto – miezi saba – huku mgonjwa mwenye umri mkubwa zaidi akiwa ni mzee wa umri wa miaka 95.

Akiongea katika Kaunti ya Embu, Bw Kagwe amesema jumla ya wagonjwa 457 wamepona; 401 miongoni mwa wakiwa ni wale ambao walikuwa wakitibiwa nyumbani na 56 walikuwa wakitibiwa hospitalini.

“Kwa hivyo, kufikia sasa (Jumamosi) jumla ya wagonjwa 4,440 wamepona nchini tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kiripotiwe nchini kwa mara ya kwanza. Vilevile, ni huzuni kwamba tumewapoteza watu wengine watatu zaidi kutokana na ugonjwa huu ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita. Kwa hivyo, kufikia sasa idadi jumla ya waliofariki ni 225,” Bw Kagwe amesema.

Na mnamo Jumamosi, Kaunti ya Tana River imeingia kwenye orodha ya kaunti ambazo zimerekodi visa vya Covid-19 nchini Kenya na hivyo kufikisha kaunti 44.