Habari

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 102

September 7th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI haijalegeza kamba sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, imesema Wizara ya Afya.

Kauli hiyo imejiri kufuatia mikutano ya hadhara ya kisiasa ambayo imeanza kuonekana ikiandaliwa na baadhi ya viongozi na wanasiasa nchini.

Waziri Msaidizi katika Wizara, Dkt Rashid Aman amesema Jumatatu kwamba marufuku ya mikusanyiko ya umma yangalipo.

Ilani ya kuzuia watu kukusanyika ni kati ya kanuni zilizotolewa ili kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

“Hatujalegeza kanuni na mikakati tuliyoweka kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu,” amesema waziri.

Amesema viongozi na wanasiasa wanaoandaa mikusanyiko ya umma, wanakiuka mikakati hiyo.

“Wanaenda kinyume na kanuni na mikakati tuliyoweka. Ni makosa. Tunawasihi watii mapendekezo tuliyoweka,” akasisitiza Dkt Aman.

Mwezi uliopita, Agosti, Rais Uhuru Kenyatta alionekana akihutubia umati mkubwa wa watu katika mtaa wa Mukuru kwa Reuben, Nairobi, baada ya kukagua miradi ya maendeleo.

Kiongozi huyo wa taifa alikuwa ameandamana na Mkuu wa Shirika la Kuimarisha Huduma za Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohammed Badi.

Viongozi wa hadhi ya juu nchini, wanasiasa na mawaziri kadhaa wameonekana wakiandaa mikutano ya umma.

Kauli ya Dkt Aman imejiri wakati ambapo kiwango cha maambukizi ya Covid-19 nchini kimeonekana kushuka.

Mnamo Jumatatu, chini ya kipindi cha saa 24 zilizopita, Kenya imethibitisha visa 102 vipya.

Idadi hiyo inafikisha jumla ya visa 35,205 vya corona nchini, tangu kisa cha kwanza kitangazwe Machi 13, 2020.