Habari Mseto

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 130

September 23rd, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WAKENYA wamepongezwa katika jitihada za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Baraza la Magavana (CoG) kupitia Kamati yake ya Afya limesema Jumatano kwamba kile kinachoonekana kama kupungua kwa kiwango cha maambukizi nchini, kinatokana na umoja wa wananchi kupambana na ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Isiolo, Mohamed Kuti amesema umma umeonekana kuchukua tahadhari kudhibiti maambukizi zaidi ukilinganishwa na viongozi.

“Tunapongeza Wakenya kwa umoja walioonyesha kusaidia katika kampeni dhidi ya Covid-19. Wamekuwa makini kuliko viongozi kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu,” Bw Kuti akasema katika kikao na wanahabari wakati Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe akitoa taarifa ya maambukizi ya corona nchini chini ya saa 24 zilizopita.

Katika kipindi cha muda wa wiki kadhaa zilizopita, kiwango cha maambukizi kimeoenekana kushuka, hatua inayoashiria afueni katika vita dhidi ya Covid-19 nchini.

Gavana huyo hata hivyo ameonya kwamba endapo watu watapuuza sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia maenezi, huenda taifa likarejea lilipotoka.

“Tukianza kutoa maski na kufeli kunawa mikono mara kwa mara…tutarudi katika hali tuliyokuwa,” Gavana Kuti akaonya.

Jumatano, chini ya saa 24 zilizopita, Wizara ya Afya imetangaza maambukizi mapya 130, kutoka kwa sampuli 3, 874, idadi hiyo ikifikisha jumla ya visa 37, 348 vya Covid-19 nchini tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza Machi 2020.

Waziri Kagwe amesema kufikia sasa jumla ya sampuli 523,998 zimekaguliwa na kufanyiwa vipimo.

Wagonjwa 106, wamethibitishwa kupona chini ya saa 24 zilizopita, takwimu hiyo ikifikisha 24,253 jumla ya wagonjwa waliopona corona nchini.

Hata hivyo, Bw Kagwe amesikitika akisema watu watano wamefariki idadi jumla ya wahanga – waliofariki – wa Covid-19 nchini ikifika 664.