Habari

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 164 idadi jumla ikifika 37,871

September 26th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA imeandikisha visa vingine 164 vya maambukizi ya Covid-19 na hivyo kufikisha 37,871 idadi jumla ya maambukizi.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari Jumamosi, Wizara ya Afya ilisema kuwa visa hivyo vipya viligunduliwa baada ya sampuli 3,872 kufanyiwa vipimo ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

“Kwa hivyo, jumla ya vipimo ambavyo vimefanywa kufikia sasa vimefikia 536,601,” taaarifa hiyo iliyotiwa saini na waziri Mutahi Kagwe ikasema.

Kulingana na taarifa hiyo, Nairobi inaongoza kwa visa vipya 41, ikifuatwa na Busia (visa 22), Kisumu (17), Turkana na Embu visa 14 kila moja.

Nayo Mombasa iliandikisha visa 11, Nakuru (10), West Pokot (6), Trans Nzoia (5), Narok (4), Machakos (4), Uasin Gishu (4), Kilifi (3), Bungoma (2), Kiambu, Marsabit ziliandikisha visa viwili kila moja huku Kakamega, Kericho, Siaya na Taita Taveta zikinakili kisa kimoja kila moja.

Bw Kagwe alisema katika kipindi hicho cha saa 24, watu 77 waliruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kupona Covid-19, hivyo kufikisha 24, 581 idadi jumla ya waliopona.

Miongoni mwao, 40 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini ilhali 37 walikuwa wakiuguzwa chini ya mpango wa utunzaji nyumbani.

Kwa bahati mbaya, watu saba zaidi walifariki kutokana na ugonjwa huo na hivyo kufikisha 689 idadi ya waliofariki tangu Machi mwaka huu.