Habari

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 24 ikiwa idadi ya juu zaidi kwa siku moja

May 2nd, 2020 1 min read

Na FAITH NYAMAI

KENYA leo Jumamosi imeripoti idadi ya juu kabisa ya visa vipya vya wagonjwa wa Covid-19 ambapo Wizara ya Afya imesema 24 hao wanafikisha idadi jumla kuwa 435 tangu kutangazwa kwa kisa cha kwanza nchini Machi 13, 2020.

Waziri Msaidizi (CAS) Dkt Mercy Mwangangi amebainisha maeneo mbalimbali ambapo wagonjwa wamepatikana.

“Hivi visa 24 vipya vya wagonjwa wa Covid-19 vimegundulika baada ya kuchukua sampuli kutoka kwa watu 1,195 na kisha kufanya vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita,” amesema Dkt Mwangangi.

Amefichua kwamba visa saba ni vya kutokea Kawangware, Nairobi, 10 mtaani Eastleigh jijini Nairobi, vitano Kaunti ya Mombasa na visa viwili vikiwa ni wagonjwa kutoka Kuria Magharibi katika Kaunti ya Migori.

Wizara imesema mgonjwa mmoja amefariki Mombasa na kufanya idadi ya wahanga kuwa 22.

Waliopona wamefika 152 baada ya serikali kueleza kwamba watu wawili zaidi wamepona maradhi hayo na hivyo kuruhusiwa kuondoka hospitalini.