Habari Mseto

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 247 idadi jumla ikifika 7,188

July 3rd, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya Ijumaa imetangaza kwamba katika kipindi cha saa 24 zilizopita watu 247 zaidi wamethibitishwa wanaugua Covid-19.

Hii ni baada ya wataalamu wa afya na huduma za maabara kuchukua sampuli 4,147 na kuzifanyia vipimo.

Waziri Msaidizi Dkt Rashid Aman amesema idadi jumla ya visa vya ugonjwa huo nchini imefika 7,188 tangu Machi 13, 2020, kufika sasa.

Katika visa vya Ijumaa, wagonjwa 242 ni Wakenya huku watano wakiwa raia wa kigeni.

“Katika visa vya leo, 164 ni jinsia ya kiume na 83 jinsia ya kike. Mgonjwa wa umri wa chini amekuwa mtoto wa mwaka mmoja, na umri wa juu miaka 100 na ambaye amekuwa wa umri wa juu zaidi kati ya visa vyote vya Covid-19 nchini,” Dkt Aman amesema.

Kaunti ya Nairobi inaendelea kuongoza katika maambukizi ambapo katika kipindi cha saa 24 zilizopita imeandikisha visa 153, Mombasa (35), Kajiado (15), Busia na Kiambu visa 12 kila moja, Garissa, Uasin Gishu na Machakos visa 4 kila kaunti.

Nazo kaunti za Murang’a, Siaya na Nakuru zimethibitisha visa viwili kila moja, nazo Nyamira na Lamu zikiwa na kisa kimoja kila kaunti.

“Ni furaha kutangaza kuwa katika muda wa saa 24 zilizopita wagonjwa 39 wameruhusiwa kuondoka katika vituo mbalimbali vya afya walipokuwa wakipokea matibabu, baada ya kuthibitishwa kupona kabisa. Idadi jumla ya waliopona Covid-19 nchini imefika 2,148. Tunaendelea kupongeza wahudumu wetu wa afya kwa jitihada zao,” akaeleza.

Wizara ya Afya pia imethibitisha katika kipindi cha saa 24 Kenya imepoteza watu wawili kutokana na virusi vya corona, jumla idadi ya walioangamizwa na Covid-19 ikigonga 154.