COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 271 idadi jumla ikipanda hadi 97,394

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 271 idadi jumla ikipanda hadi 97,394

Na CHARLES WASONGA

KENYA Jumatano imenakili visa 271 zaidi vya maambukizi ya Covid-19 na hivyo kufikisha idadi jumla ya maambukizi kuwa 97,394.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya janga hilo nchini, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kuwa wagonjwa hao wapya walipatikana baada ya sampuli kutoka watu 5,830 kupimwa ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

Hiyo inawakilisha kiwango cha maambukizi cha asilimia 4.6 na Nairobi inaongoza kwa kuandikisha visa 117 vya corona.

Kufikia Jumatano Januari 6, 2021, idadi ya sampuli ambazo zimepimwa tangu janga hilo lilipogunduliwa nchini kwa mara ya kwanza Machi 13, 2020 ni 1,070,249.

Na idadi ya maafa kutokana na Covid-19 imeongezeka hadi 1,694 baada ya wagonjwa wanne kufariki.

Nazo habari njema ni kwamba jumla ya wagonjwa 609 walithibitishwa kupona corona ndani ya saa 24 ambapo jumla ya wagonjwa 502 walikuwa wakiuuguzwa nyumbani na wengine 107 walikuwa wamelazwa hospitalini.

“Kwa hivyo, kufikia sasa (Jumatano) idadi jumla ya wagonjwa wa Covid-19 waliopona na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida ni 79,966,” akasema Bw Kagwe.

Waziri aliongeza kuwa jumla ya wagonjwa 588 wa corona wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku wengine 2,708 wakiuguzwa chini ya mpango wa utunzaji nyumbani.

“Jumla ya wagonjwa 27 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) huku wengine 16 wakiongezwa hewa na oksijeni,” akaongeza.

You can share this post!

Wezi wajipikia ugali, nyama na kushukuru familia kwa...

Kocha Nuno Espirito wa Wolves atozwa faini ya Sh3.5 milioni...