Habari Mseto

Covid-19: Kibra yapata visa vingi zaidi

May 28th, 2020 1 min read

NA MWANDISHI WETU

MTAA wa Kibra Alhamisi umerekodi idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa virusi vya corona, kati ya mitaa ya jiji la Nairobi huku taifa likiendelea kupima watu wengi.

Mtaa huo ambao ni maskani ya maelfu ya wakazi umepata visa 35, hofu ikiibuka kuwa huenda ugonjwa huo ukasambaa zaidi miongoni mwa mitaa duni.

Idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo Alhamisi ni 147 huku idadi kamili ya wanaougua Covid-19 ikifikia watu 1618 kote nchini. Kati ya hao 147 ni mtoto wa mwaka mmoja.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe akitoa hotuba ya kila siku katika kaunti ya Kiambu alisema kwamba idadi hiyo inaendelea kupanda huku watu 3 zaidi wakifariki na kufikisha 58 idadi ya waliofariki kutokana na janga hilo.

Watu walioruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupona corona imefikia watu 421.

“Tunapaswa kuchukulia janga hili kwa makini kwa sababu idadi inaendelea kuongezeka,” alisema Bw Kagwe katika ziara yake ya Kaunti ya Kiambu.

Kaunti za Nyeri na Uasin Gishu zimerekodi visa 2 huku Embu, Homabay, Murang’a, Machakos na Kijiado zikirekodi kisa kimoja kila moja.