COVID-19: Kocha Jurgen Klopp akosa kusafiri Ujerumani kuhudhuria mazishi ya mama yake mzazi

COVID-19: Kocha Jurgen Klopp akosa kusafiri Ujerumani kuhudhuria mazishi ya mama yake mzazi

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp hakuweza kurejea nchini Ujerumani kwa minajili ya mazishi ya mamaye mzazi mnamo Februari 10 kwa sababu ya masharti makali ya kudhibiti msambao wa virusi vya corona nchini humo.

Ujerumani imepiga marufuku safari zote za nje kutoka mataifa yanayoshuhudia maambukizi mapya ya Covid-19, ikiwemo Uingereza anakofanyia kazi Klopp.

Kupitia akaunti yao ya mtandao wa Twitter, Liverpool walitumia Klopp ujumbe wa kumfariji mnamo Jumatano uliosema: “Hutawahi kutembea peke yako Jurgen.”

Akihojiwa na gazeti la Schwarzwalder Bote nchini Ujerumani, Klopp alisema mama yake mzazi alikuwa “kila kitu kwake na alimaanisha mengi maishani mwake”.

“Alikuwa mama niliyemstahi sana kwa pendo halisi. Sina neon jema na bora zaidi la kuelezea uzuri wake kwangu. Hata hivyo, ugumu wa hali inayopitiwa kwa sasa duniani kote kwa sababu ya Covid-19 ulinifanya kutohudhuria mazishi yake,” akatanguliza.

“Mambo yatakapotengenea, naahidi kusafiri Ujerumani kuandaa hafla ya kukumbuka yote mema aliyonifanyia mamangu katika uhai wake,” akaeleza kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.

Wakijibu ujumbe aliotumiwa na Liverpool, vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) walisema: “Tunatuma rambirambi zetu kwa familia nzima ya Klopp, marafiki zake na wote walioguswa na msiba huo kwa namna moja au nyingine. Tunamweka Jurgen katika mawazo yetu wakati huu mgumu.”

Baadhi ya klabu ambazo pia zilituma rambirambi na jumbe la kumliwaza Klopp ni Arsenal, Manchester United, Tottenham, Atletico Madrid na Barcelona.

Masharti makali ya kudhibiti maambukizi mapya ya Covid-19 nchini Ujerumani yalichochea vinara wa Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) kuratibu michuano ya mkondo wa kwanza katika hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kati ya RB Leipzig na Liverpool kisha Borussia Monchengladbach na Manchester City kupigiwa jijini Budapest, Hungary wiki ijayo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu za lugha kama...

Macho kwa Cheptai kivumbi kikinukia kwenye mbio za nyika za...