Michezo

COVID-19: Kombe la Enterprise kutupwa kando kupisha raga ya Kenya Cup

May 7th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha Enterprise Cup kitafutiliwa mbali katika kalenda ya raga ya humu nchini msimu huu ili kuwezesha vikosi kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Kenya Cup.

Pendekezo hili la wasimamizi wa klabu mbalimbali linatarajiwa kuidhinishwa na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) ambao wamebatilisha maamuzi ya awali ya kufutilia mbali kabisa msimu huu mzima wa raga kutokana na janga la corona.

Hadi kusitishwa kwa shughuli zote za michezo humu nchini mnamo Machi 2020, kivumbi cha Enterprise Cup ambacho ndicho cha zamani zaidi katika historia ya raga ya Kenya, kilikuwa kimetinga hatua ya nusu-fainali.

Mabingwa watetezi Kabras RFC walikuwa wamepangwa kuvaana na Homeboyz huku wanabenki wa KCB wakiratibiwa kumenyana na Impala Saracens.

Kwa mujibu wa KRU, itakuwa busara kufutilia mbali kipute cha Enterprise Cup ili kupunguza mrundiko wa mechi katika kalenda ya msimu huu pindi michuano ya raga ya Kenya Cup itakaporejelewa baada ya corona kudhibitiwa vilivyo.

Kwa mujibu wa Xavier Makuba ambaye ni mwenyekiti wa kivumbi cha Kenya Cup, kinyang’anyiro hicho kimeratibiwa kurejelewa mnamo Julai 2020 na maamuzi hayo yamechochewa na ukubwa wa kiwango cha fedha zilizowekezwa kwa minajili ya mapambano hayo.

Kinyume na washikadau wengine, Makuba ametaka klabu husika kuwapa wanaraga wao muda wa hadi wiki tatu pekee za kujiandaa kwa mchujo wa Kenya Cup kisha fainali ya mashindano hayo.

“Sidhani tutahitaji wiki sita za kujiandaa kwa mechi zilizosalia msimu huu. Majuma matatu yanatosha wachezaji kupiga kambi na kujifua vilivyo kwa kibarua kilichopo mbele yao,” akatanguliza Makuba.

“Nina imani msimu huu wa Kenya Cup utakamilika kwa wakati ufaao na kupisha mapambano ya Raga ya Kitaifa ya Sevens Circuit. Iwapo mambo yawiana na mipangilio yetu na klabu zote zishirikiane nasi, basi sioni lolote litakalotuzuia kutamatisha rasmi kampeni za raga ya msimu huu kufikia katikati ya Julai,” akaongeza.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa kwa kamati ya KRU inayosimamia ratiba za mechi za Kenya Cup chini ya uenyekiti wa Hillary Itela anayetazamiwa kutoa maamuzi yao mwishoni mwa wiki hii.

Homeboyz walitarajiwa kuchuana na Menengai Oilers ambapo mshindi angejikatia tiketi ya kukabiliana na mabingwa watetezi, KCB katika hatua ya nusu-fainali ya Kenya Cup. Kabras walitazamiwa kupimana ubabe na mshindi kati ya Impala na Mwamba RFC.

Hadi kufutiliwa mbali kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup, Kabras ya kocha Henley Du Plessis ilikuwa ikiselelea kileleni kwa alama 74, tatu zaidi mbele ya KCB.

Janga la corona limeathiri pia kivumbi cha KRU Championship, ligi pana za kitaifa, ligi zote za madaraja ya chini, kipute cha Great Rift Valley Cup, Mwamba Cup na ligi ya kitaifa ya National Cirucit.

Kwa upande wa KRU Championship, Strathmore Leos waliokuwa hawajapoteza mechi yoyote, walikuwa wakiongoza jedwali kwa alama 76, tisa zaidi kuliko Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) katika nafasi ya pili.

Leos walikuwa wakutane na mshindi kati ya Northern Suburbs na Chuo Kikuu cha USIU-A katika mojawapo ya nusu-fainali huku MMUST wakipambana na mshindi kati ya Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Egerton Wasps.