Kimataifa

COVID-19: Korea Kusini yafunga tena shule baada ya kuzuka kwa wimbi la pili la maambukizi

May 30th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

SEOUL, Korea Kusini

HUKU mjadala kuhusu iwapo shule nchini Kenya zifunguliwe au la kabla ya Covid-19 kudhibitiwa kabisa, zaidi ya shule 500 nchini Korea Kusini zimefungwa muda mfupi baada ya kufunguliwa.

Hii ni baada ya kuzuka kwa wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona katika jiji kuu Seol na maeneo ya karibu.

Aidha, kumbi za maonyesha ya vyombo vya sanaa na michezo ya kuigiza na makavazi ya serikali jijini humo pia zimefungwa kwa muda wa wiki mbili.

Waziri wa Afya Park Neung-hoo pia alisema kuwa serikali serikali imeamuru kufungwa kwa shule za kibinafsi na vituo vya kusakura mitandao ya intanet hadi Juni 14.

Park pia aliwataka wakazi wa Seoul na maeneo ya karibu wakome kutoa nje au kushiriki hafla zozote kwa kipindi cha majuma mawili.

Mlipuko mpya wa virusi vya corona uliripoti katika kituo kimoja cha usambazaji bidhaa mbalimbali katika kitongoji cha Bucheon. Takriban visa 100 vya vya maambukizi viliripotiwa katika kituo hicho Ijumaa, kulingana na taarifa iliyotolewa na Naibu Waziri wa Afya Kim Gang-lip.

Aliongeza kuwa kufikia sasa Jumamosi jumla ya watu 3,836 kati ya wafanyakazi 4,351 na wageni walikuwa wamepimwa virusi vya corona katika kituo hicho.

Korea Kusini imekuwa akichukuliwa kama taifa la kupigiwa mfano kuhusiana na jinsi ya kupunguza kuenea kwa virusi vya corona bila kuzima shughuli za kiuchumi.

Hii ni kutokana na uwezo wake wa kuendesha upimaji wa watu wengi kwa muda mfupi, kuwasaka waliotangamana na wagonjwa wa Covid-19 na kuwapa matibabu au kuwazuia katika vituo vya karantini.

Kufikia Alhamisi wiki hii jumla ya shule 838 katika maeneo mengine nchini humo zilikuwa zimeahirisha ufunguzi huku wanafunzi wakishauriwa kuendelea na vipindi vya masomo kupitia mitandaoni.

Hadi Ijumaa, idadi jumla ya visa vya Covid-19 nchini Korea Kusini ilikuwa 11,402. Watu 268 wamefariki kutoka na homa hiyo huku wagonjwa 770 waliendelea kuhudumiwa katika wadi maalum zilizotengewa mahsusi kwa ugonjwa huo.