Kimataifa

COVID-19: Madereva wanane kutoka nchini Tanzania wazimwa kuingia Kenya

May 15th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MEDEREVA wanane wa matrela kutoka Tanzania wamezuiwa kuingia nchini Kenya baada ya kupatikana na virusi vya corona katika mji wa mpakani wa Namanga.

Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi alisema Alhamisi kurunzi ya serikali sasa inaelekezwa katika maeneo ya mipaka na hasa mji huo ulioko kwenye mpaka baina ya Kenya na Tanzania.

“Maeneo ya mipaka yetu yenye mianya mingi ya kuingia hivi karibuni yameshuhudia ongezeko kubwa la maambukizi ya Covid-19. Madereva ya matrela ndio wanarudisha nyuma vita dhidi ya kusambaa kwa virusi hivi,” akasema.

Dkt Mwangangi alisema Kenya imelalamikia mienendo ya wageni kuingia kupitia maeneo ya mpakana yasiyo rasmi lakini akatoa hakikisho kuwa serikali inajadiliana na mataifa jirani kuhusu njia za kusuluhisha shida hiyo.

Alisema Kamati ya Kitaifa kuhusu Janga la Covid-19 inafuatilia suala hilo na itachukua hatua zifaazo.

“Ningependa kuwahimiza Wakenya kuwa watulivu kwani serikali inashughulikia hali hiyo,” Dkt Mwangangi akasema.

Waziri huyo msaidizi alizitaka jamii zinazoishi karibu na maeneo ya mpaka kuweka doria za kiusalama chini ya mpango wa Nyumba Kumi ili kuzuia raia wa kigeni kuingia nchini kinyume cha sheria.

Dkt Mwangangi aliwataka watu wa jamii hizo kutoa ripoti kwa maafisa wa usalama endapo watawaona watu wanaowashuku wakiingia nchini kutumia njia za vichochoro.

Mji wa Namanga uliorodheshwa kama kitovu cha maambukizi ya virusi vya corona mnamo Mei 14, 2020, baada ya madereva 25 kupatikana na virusi vya corona.

Mnamo Jumatano, waziri msaidizi katika Wizara ya Afya Rashid Aman alitangaza kuwa vituo vya maabara ya kuhamahama vitapelekwa Namanga kufanikisha upimaji wa Covid-19.