Habari Mseto

COVID-19: Makanisa Thika yanyunyuziwa dawa

July 15th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

IDARA ya afya ya umma imeanza shughuli ya kunyunyuzia dawa ya kukabili viini katika makanisa mjini Thika kipindi hiki ambapo dunia nzima inakabiliwa na maradhi ya Covid-19.

Afisa mkuu wa afya ya umma mjini Thika Dkt Samuel Mureithi alisema Jumanne kwamba hiyo ni mojawapo ya mikakati ya kufanya maandalizi ya ufunguzi wa makanisa baada ya kusalia yamefungwa miezi kadhaa.

“Tunajua serikali ilisema sehemu za ibada zifunguliwa lakini kwa kuzingatia masharti,” alisema Dkt Mureithi.

Maafisa hao walianza shughuli hiyo katika makanisa ya St Francis Catholic Thika, St Francis of Assisi ya Athena, na St Peter’s the Rock.

Alisema maabadi mengi yananatarajiwa kufungua milango Jumapili, Julai 19, 2020.

Alieleza kuwa baada ya kunyunyuzia dawa, maafisa hao wa afya watashirikiana na wachungaji popote walipo ili kushauriana jinsi washirika wao watavyoketi makanisani.

“Ni lazima kuweka nafasi ya mita moja au zaidi ili waumini wasikaribiane. Tutahakikisha tunapanga kazi hiyo tukishirikiana nao,” alisema Dkt Mureithi.

Hivi majuzi katika kongamano la wachungaji mjini Thika la kutathmini hali ilivyo waliohudhuria walilalamika ya kwamba pendekezo la serikali ya washirika 100 pekee kuruhusiwa kuabudu limewakera sana. Walidai ya kwamba washirika wengi wangetaka kumuabudu Mungu wakiwa kanisani na “kuambiwa wasije ni kuwakataza imani yao.”

Serikali pia ilisema wazee wa umri wa miaka 58 na zaidi pamoja na watoto wa umri wa miaka 13 kwenda nchini wasihudhurie ibada katika maabadi.

Baadhi ya masharti muhimu yaliyowekwa na Wizara ya Afya ni kunawa mikono kila mara, kuvalia barakoa, kuweka nafasi ya mita moja kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwenzake. Kingine cha muhimu pia kitakuwa ni kupima watu hali ya joto mwilini hasa katika maeneo ya hadhara kama kanisani, supamaketi, na katika ofisi za umma.