COVID-19: Manchester City kukosa masogora watano wa haiba kubwa dhidi ya Chelsea katika EPL

COVID-19: Manchester City kukosa masogora watano wa haiba kubwa dhidi ya Chelsea katika EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City watakosa huduma za wanasoka watano tegemeo watakapowaendea Chelsea kwa minajili ya mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Stamford Bridge mnamo Januari 3, 2021.

Kocha Pep Guardiola wa Man-City amethibitisha tukio hilo na kutetea pakubwa maamuzi ya kuahirishwa kwa mechi ya awali ya EPL iliyokuwa iwakutanishe na Everton mnamo Disemba 28, 2020.

Mnamo Disemba 25, Man-City walifichua visa vinne vya maambukizi ya Covid-19 kambini mwao na viwili kati ya visa hivyo vilikuwa vikihusu wanasoka Kyle Walker na Gabriel Jesus.

Vipimo zaidi vilivyofanywa mnamo Disemba 28 vilifichua visa vingine vitatu vya maambukizi miongoni mwa wachezaji ugani Etihad, hali iliyochangia kuahirishwa kwa mechi ya EPL kati ya Man-City na Everton saa chache kabla ya muda uliokuwa umeratibiwa awali.

“Wachezaji watano kwa sasa wamejitenga kwa kipindi cha siku 10 zijazo. Baadhi yao ni wale wawili waliopatikana siku ya Krismasi ambapo visa vinne viliripotiwa kambini mwetu. Sasa wachezaji watatu zaidi wameugua Covid-19 kutokana na vipimo vya hivi karibuni,” akasema Guardiola.

Man-City hata hivyo haijafichua majina ya wanasoka hao watatu wa hivi karibuni ambao kwa sasa watakosa pia mechi ya nusu-fainali ya Carabao Cuo dhidi ya watani wao wakuu Manchester United mnamo Januari 6, 2021.

Maamuzi ya kuahirishwa kwa gozi la EPL kati ya Everton na Man-City ugani Goodison Park yalikosolewa pakubwa na usimamizi wa Everton chini ya kocha Carlo Ancelotti kwa kuwa kocha Guardiola alikuwa akijivunia huduma za wachezaji 14 wa kikosi cha kwanza ambao wangenogesha mechi hiyo.

You can share this post!

Jeraha kumweka Coutinho nje kwa miezi mitano na kuweka...

Kocha Pochettino kumsajili Dele Alli mwezi huu wa Januari...