Habari

COVID-19: Maombi ya kitaifa yafanyika Ikulu

March 21st, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MAOMBI ya kitaifa kutaka Mungu ainusuru Kenya na dunia nzima inayokabiliwa na janga la Covid-19 yanaendelea katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi.

Taarifa na ujumbe unaoandamana na nyimbo za kutakasa taifa, zimetolewa na wahubiri wa madhehebu mbalimbali walioalikwa na vilevile wataalamu wa dini ya Kiislamu waliotoa dua.

Kwenye maombi, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, ACK Joseph Ole Sapit akitumia mifano kadhaa ya Biblia, ameeleza haja ya watu kuelekeza mahitaji yao kwa Mwenyezi Mungu, akitaja kwamba “kwa kiasi fulani tumesahau Mungu ndiye muweza wa yote”.

“Tunajitenga, ni muhimu kumrejea Mwenyezi Mungu, ili atuepushie majanga tunayopitia; Covid-19 na nzige ambao wameshambulia mashamba, mimea na mazao yetu,” amesema Askofu huyo kwenye sala zake.

Ole Sapit pia amesisitiza umuhimu wa kuomba msamaha kutoka kwa Mungu, kwa makosa tunayoweza kuwa tumeyafanya kwa njia ya maongezi na hata matunda.

Aidha, ametaja donda ndugu la ufisadi, siasa za chuki na ukabila, kama mambo yanayofaa kuangaziwa na suluhu kupatikana ili kuunganisha taifa.

Rais Uhuru Kenyatta na ambaye anayaongoza, alitangaza kutenga leo, Jumamosi, iwe siku ya maombi ya kitaifa.

Naibu wa Rais Dkt William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), na viongozi wakuu serikalini pia wamehudhuria maombi hayo yanayopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.

Kufikia sasa Kenya imethibitisha kuwa na visa saba vya maambukizi ya virusi hatari vya corona.