COVID-19: Mechi za Europa League kati ya Real Sociedad na Man-United na nyingine kati ya Benfica na Arsenal sasa kuchezewa nchini Italia

COVID-19: Mechi za Europa League kati ya Real Sociedad na Man-United na nyingine kati ya Benfica na Arsenal sasa kuchezewa nchini Italia

Na MASHIRIKA

MECHI ya mkondo wa kwanza ya Europa League kati ya Real Sociedad na Manchester United wiki ijayo sasa itachezewa jijini Turin, Italia badala ya Uhispania jinsi ilivyokuwa imeratibiwa awali.

Hii ni baada ya serikali ya Uhispania kuzuia safari za wageni kutoka mataifa yanayoshuhudia visa vya maambukizi mapya ya virusi vya corona.

Kanuni hiyo mpya inamaanisha kwamba Sociedad almaarufu Basque hawataweza kuandaa mechi ya hatua ya 32-bora kati yao na Man-United mnamo Alhamisi ya Februari 18, 2021.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United watakuwa wenyeji wa mkondo wa pili utakaotandaziwa ugani Old Trafford wiki moja baadaye.

Mechi ya Februari 18 itakuwa ya tatu mfululizo kwa Man-United kuchezea katika uwanja usiokuwa nyumbani kwa wapinzani wao kwenye Uropa League.

Mnamo 2019-20, miamba hao wa soka ya Uingereza walipigia mechi zao za robo-fainali na nusu-fainali kwenye Europa League dhidi ya FC Copenhagen ya Denmark na Sevilla ya Uhispania jijini Cologne, Ujerumani.

Mpangilio huo ulichochewa na mkurupuko wa janga la corona lililovuruga pakubwa ratiba ya kivumbi hicho kilichofanywa kuwa cha mkondo mmoja pekee kuanzia hatua ya robo-fainali.

Kwingineko, mechi zote za mikondo miwili kati ya Arsenal na Benfica ya Ureno zitachezewa sasa uwanjani Olimpico jijini Roma, Italia.

Tottenham Hotspur na Leicester City ambao ni wawakilishi wengine wa soka ya Uingereza kwenye Europa League muhula huu hawajaathiriwa.

Kocha Jose Mourinho anatarajiwa kuongoza kikosi chake cha Spurs kupepetana na Wolfsberger kwenye mkondo wa kwanza nchini Austria huku Leicester ya kocha Brendan Rodgers ikitazamiwa kufunga safari ya kuelekea jijini Prague katika Jamhuri ya Czech kumenyana na Slavia.

Katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), gozi la mkondo wa kwanza katika hatua ya 16-bora kati ya Chelsea na Atletico Madrid ya Uhispania litatandaziwa ama Bucharest (Romania) au Warsaw (Poland).

Yalikuwa matarajio ya Atletico wanaonolewa na kocha Diego Simeone kuchuma nafuu ya kucheza dhidi ya Chelsea katika uwanja wao wa nyumbani wa Wanda Metropolitano.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Atletico watapania kupepetana na Chelsea uwanjani Arena Nationala jijini Bucharest. Huko ndiko ambako Atletico waliwahi kuwacharaza Athletic Bilbao waliokuwa wakitiwa makali na kocha Marcelo Bielsa na kunyanyua taji la Europa League mnamo 2012.

Vinara wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) tayari wamethibitisha kwamba mechi za mkondo wa kwanza katika hatua ya 16-bora ya UEFA kati ya RB Leipzig na Liverpool na nyingine kati ya Borussia Monchengladbach na Manchester City zitachezewa jijini Budapest, Hungary.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Elimu: Mtaala mpya wahitaji ushirikiano

Real Madrid wapiga Getafe na kukaribia Atletico kileleni...